Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

UZINGATIWAJI WA MAADILI NI KIGEZO CHA UTOAJI WA HUDUMA BORA KWA JAMII -MSAJILI.

Posted on: March 22nd, 2024



Na WAF, DODOMA.

Wataalam wa Optometria nchini wameaswa kuwa mstari wa mbele kuzingatia Madili na weledi wakati wa utoaji huduma na wakati usio wa kazi hali itakayoongeza imani kwa jamii na kuwawezesha kutimiza wajibu wao ipasavyo.

Kauli hiyo, imetolewa Machi 22, 2024 jijini Dodoma na Msajili wa Baraza la Optometria Sebastiano Millanzi wakati wa hafla yakuwajengea uwezo na kuwapatia vyeti wataalam waliosoma vyuo ya KCMC, Mvumi na nje ya Nchi wapatao
72 ambapo miongoni mwao walipata usajili kamili na wengine usajili wa muda.

"Kutunza siri za Mgonjwa iwe kipaumbele chenu, sio unamtibu mtu kisha unakwenda kutoa taarifa zake mitaani" amesema Millanzi na kuongeza kuwa mbali na kutunza siri lakini suala la haiba ni muhimu kuzingatiwa.

Millanzi amewasisitiza wataalam hao kuhusu Lugha ya staha, Mavazi, Nywele, kutojihusisha na rushwa kwa wale watakaofanikiwa kufanya kazi katika vituo vya umma na vituo binafsi.

"Tangulizeni utu, kabla ya vitu, huo ndio uzalendo na wito kwa kazi ambayo umeitiwa, mtakutana na watu wanaohitaji na ukimwangali hajiwezi, kwanza okoa maisha yake ndio mambo mengine yafuate" amesema Millanzi.

Pia Millanzi aliwaasa wataalam kuzingatia utoaji wa rufaa haraka hasa kwa wagonjwa watakaokuwa na sifa ya kupewa rufaa
"kumekuwa na tabia ya baadhi ya wataalam wa Optometria kuwakumbatia wagonjwa pasipo sababu za msingi, hali ambayo inaweza kuwasababishia wagonjwa madhara makubwa kama ulemavu wa kutokuona", amesisitiza Msajili Millanzi.

Kwa Upande wake Afisa Usajili, bi Anna Josephat kutoka Baraza la Usajili amewaonya wataalam hao kuepuka ulevi uliokithiri kwani utawaharibia kazi na kufanya wasiaminike na jamii.

"Tunajua miongoni mwenu wapo watakaojiajiri au kuajiriwa, rai yangu kwenu muwe na utimamu muda wote mnapofikiwa na wateja, sio mgonjwa anakuja anakukuta umeeewa" Amesema bi Anna.

Wakati wa Michango yao wataalama hao walikiri, kwenda kuzingatia Maadili ya kazi yao.

MWISHO