Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

UWEKEZAJI WA BILIONI 38 MKOMBOZI WA SARATANI NCHINI

Posted on: March 19th, 2025

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI imepongeza juhudi za Serikali katika mapambano dhidi ya saratani, hasa kupitia uwekezaji wa Shilingi Bilioni 38 kwenye ujenzi wa jengo jipya la matibabu ya saratani katika Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo jijini Dodoma, ambalo hadi sasa limekamilika kwa asilimia 57.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Hassan Mtenga, amesema ujenzi wa hospitali hiyo mpya ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kuhakikisha huduma bora za matibabu ya saratani zinapatikana katika maeneo mengi zaidi nchini kwani uwekezaji huo unalenga kupunguza mzigo mkubwa wa wagonjwa wanaotegemea Hospitali ya Ocean Road jijini Dar es Salaam.

"Kumekuwa na upotoshaji kuhusu uwekezaji wa Serikali katika sekta ya afya, lakini ukweli ni kwamba Rais Samia amesimama imara kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora. Wagonjwa wa saratani sasa wana nafasi kubwa ya kupata nafuu na hii ni kutokana na uwekezaji huu ambao unafanyika hapa na itakapokamilika hakutakuwa na haja ya kwenda kujazana Dar es Salaam kwa ajili kupata matibabu ya Saratani," amesema Mhe. Mtenga.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, amesema maboresho yanayoendelea yamewezesha asilimia 78 ya wagonjwa wa saratani kupata nafuu kutokana na ugunduzi wa mapema wa ugonjwa huo, kwani kutokana teknolojia iliyopo kwa sasa ina uwezo wa kugundua ugonjwa huo hata miaka 10 kabla ya kujitokeza.

“Leo hii, tuna uwezo wa kugundua saratani mapema sana, jambo linalosaidia matibabu kwa wakati na kuokoa maisha ya maelfu ya Watanzania. Uwekezaji huu ni hatua kubwa katika sekta ya afya,” amesema Dkt. Mollel.

Serikali imewekeza zaidi ya Shilingi Trilioni 6.7 katika maboresho ya sekta ya afya kwa miaka minne, ikiwa ni jitihada za kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora zaidi za matibabu nchini.