UTEKELEZAJI WA BIMA YA AFYA KWA WOTE UENDE SAMBAMBA NA UBORA WA HUDUMA
Posted on: December 20th, 2025Na WAF Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Mohammed Mchengerwa, amewataka viongozi na watendaji wa Sekta ya Afya nchini kuhakikisha utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ya mwaka 2023 unakwenda sambamba na utoaji wa huduma bora, zenye utu na zisizo na ubaguzi kwa wananchi.
Dkt. Samizi ameyasema hayo Desemba 18, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa kikao cha viongozi wa sekta ya afya kilicholenga kutoa taarifa ya hatua iliyofikiwa katika maandalizi ya utekelezaji wa sheria hiyo, akibainisha kuwa maandalizi muhimu yamekamilika kabla ya kuanza usajili rasmi wa wananchi katika mfumo wa bima ya afya kwa wote.
Amesema utekelezaji wa mpango huo ni sehemu ya kutafsiri maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha huduma za afya zinamfuata mwananchi badala ya mwananchi kuzifuata huduma, sambamba na kauli mbiu ya “Kazi na Utu, Tunasonga Mbele.”
Akizungumza kuhusu maandalizi ya Serikali, Dkt. Samizi amesema Serikali imeendelea kuimarisha mazingira wezeshi katika sekta ya afya kwa kuongeza ajira za watumishi wa afya, kujenga na kukarabati vituo vya kutolea huduma za afya, kuboresha upatikanaji wa dawa pamoja na kununua na kusimikwa kwa vifaa tiba na vifaa vya kisasa.
Ameeleza kuwa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote inaweka msisitizo wa kila mwananchi kuwa na bima ya afya itakayomuwezesha kumudu gharama za matibabu na kupata huduma kwa uhakika pindi anapozihitaji, huku akisisitiza kuwa jukumu la watendaji wa sekta ya afya ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kwa wakati.