Wizara Ya Afya

USHIRIKIANO WA MAABARA TANZANIA BARA NA ZANZIBAR KUIMARISHA UTAYARI DHIDI YA MAGONJWA YA MLIPUKO

Posted on: July 10th, 2026

Na Mwandishi Wetu, WAF – Zanzibar

Serikali kupitia Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii imeendelea kuimarisha ushirikiano wa kitaalamu kati ya Tanzania Bara na Zanzibar ili kujenga mfumo madhubuti wa maabara utakaoongeza uwezo wa taifa katika kugundua, kuthibitisha na kudhibiti magonjwa ya mlipuko kwa wakati.

Hayo yamesemwa leo, Julai 10, 2026, na Mkurugenzi wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii, Bw. Ambele Mwafulango, wakati wa ziara maalumu ya Watendaji wa Maabara ya Afya ya Jamii Tanzania Bara katika Wizara ya Afya Zanzibar, iliyolenga kujadili fursa za kuboresha ushirikiano wa kitaalamu na kubadilishana uzoefu katika huduma za maabara.

Bw. Mwafulango amesema ushirikiano huo utasaidia kuoanisha viwango vya ubora wa huduma za maabara, kuongeza matumizi ya teknolojia za kisasa, kuimarisha uwezo wa wataalamu kupitia mafunzo ya pamoja na kuboresha mifumo ya uchunguzi wa magonjwa ya mlipuko nchini.

“Ziara hii ni sehemu ya jitihada endelevu za Serikali za kuimarisha ushirikiano wa kitaalamu kati ya Tanzania Bara na Zanzibar ili kuhakikisha mifumo ya uchunguzi na mwitikio dhidi ya magonjwa ya mlipuko inaendelea kuwa imara na yenye uwezo wa kulinda afya za wananchi na taifa kwa ujumla,” amesema Bw. Mwafulango.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya kinga kutoka Wizara ya Afya Zanzibar, Dkt. Salim, amesema Zanzibar itaendelea kushirikiana kwa karibu na Tanzania Bara katika kubadilishana taarifa za kitaalamu, kufanya tafiti na kuendeleza programu za pamoja zitakazoongeza utayari wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko, ikiwemo Ebola na magonjwa mengine ya kuambukiza.

Ameongeza kuwa ushirikiano huo utaimarisha uratibu wa kitaifa katika sekta ya maabara, kurahisisha mwitikio wa pamoja wakati wa dharura za afya na kuweka msingi imara wa kujenga mfumo endelevu wa usalama wa afya nchini.