USHIRIKIANO SEKTA YA UMMA, BINAFSI WATAKIWA ILI KUBORESHA HUDUMA ZA SARATANI NCHINI
Posted on: October 17th, 2024
Na WAF, DSM
Serikali imesisitiza umuhimu wa sekta ya Umma na binafsi kushirikiana ili kuboresha huduma za matibabu ya saratani nchini.
Wito huo umetolewa leo Oktoba 16, 2024 na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu alipokutana na uongozi wa Hospitali na Chuo Kikuu cha Aga Khan Tanzania kwa lengo la kujadili kuhusu Mradi wa Kuendeleza Huduma za Saratani nchini
Prof. Nagu amesema mradi huo unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania(GoT), Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN), Benki ya Maendeleo ya Ufaransa(AFD) na Taasisi ya Bill & Melinda Gates Foundation(BMGF), utajikita zaidi kwenye ugunduzi wa mapema na matibabu ya saratani, hususani saratani ya matiti na saratani ya mlango wa kizazi.
Prof. Nagu ametumia wasaa huo kuipongeza Taasisi ya Aghakhan Tanzania kwa usimamizi mzuri wa mradi wa awamu ya kwanza ambao muda wake umemalizika.
Prof. Nagu amekaribisha na kusifu hatua hii ya upembuzi wa awamu ya pili ya manufaa ya mradi huu na kuhimiza kuwa huu ndio mwelekeo wa Serikali wa kushirikiana na taasisi binafsi katika kuendeleza huduma za Afya nchini.
Katika mwendelezo wa awamu ya pili wa mradi huu wa saratani, Mganga Mkuu wa Serikali amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha kuwa mradi huo unafikiwa na wengi hususani ni kupitia utekelezaji wa Bima ya Afya kwa wote.
“Mradi unapaswa kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kuimarisha miundombinu ya matibabu ya saratani iliyokwisha anzishwa nchini, kabla ya kuanza miradi mipya,” amefafanua Prof. Nagu.
Amesisitiza pia kuhusu umuhimu wa kuwekeza kwenye ubora wa huduma hususani katika uanzishwaji wa bodi za ithibati na uaandaaji miongozo ya matibabu ikiwemo matibabu ya saratani nchini (Standard Management Guideline and Standard Operating Procedure for referrals).
Aidha Prof. Nagu amesema jamii inapaswa kushirikishwa ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo watumishi wa afya ngazi ya jamii (CHWs).