Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

UONGOZI WA TAASISI YA OCEAN ROAD WAMKOSHA DKT. MOLLEL

Posted on: October 9th, 2023



Na. WAF, Dar Es Salaam

Naibu Waziri wa Afya Dkt Godwin Mollel amewapongeza na kuwatia moyo Menejimenti na watumishi wa Taasisi ya Saratani Ocean Road kwa kazi nzuri ya kuwahudumia wananchi na usimamiaji wa utekelezaji miradi ya uboreshaji wa miundombinu ya kutolea Huduma za afya inayoletwa na serikali.


Dkt. Mollel ametoa pongezi hizo Jijini Dar Es Salaam wakati alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma za Afya kwa wananchi na kuongea na menejimenti ya watumishi wa Taasisi ya Saratani Ocean Road.


Dkt.Mollel amesema kuwa uongozi imara wa menejimenti ya Taasisi ya Saratani Ocean Road ndo matokeo chanya ya ujenzi wa jengo la mradi wa PET-CT Scan na Cyclotron unaogharimu kiasi cha shilingi Bilioni 18.2 ili kuleta tija ya uwekezaji uliofanywa na serikali kwa wananchi.


“Utekelezaji wa mradi wa wa PET-CT Scan na Cyclotron mpaka sasa umekamilika kwa asilimia 98 ambapo Mashine tayari zimekwishasimikwa kwa asilimia 100 huku wakisubiri utaratibu wa kuunganisha umeme pekee ili mashine hizo zianze kutumika kama inavyotakiwa”, ameeleza Dkt. Mollel


Vile vile amesema jengo hilo limekusanya mashine mbili kubwa ambazo ni kiwanda cha kutengeneza mionzi ambapo kwa sasa kwa Tanzania nzima kitakuwa ni kimoja tu ambacho kitakuwa kikitengeneza mionzi ambayo itatumika kwa Taasisi huku mingine ikipelekwa kwenye hospitali nyingine kwaajili ya kusaidia wahanga wa huko.