UCHUNGUZI WA SAMPULI WAONGEZEKA KWA ASILIMIA 21
Posted on: March 15th, 2025
Na. WAF, Dodoma
Serikali imeimarisha upatikanaji wa huduma za kiuchunguzi wa Kisayansi wa kimaabara kwa sampuli na kufanya ongezeko la asilimia 21 kutoka sampuli 155,817 Mwaka Fedha 2021/2022 hadi kufikia sampuli 188,362 kwa mwaka wa Fedha 2023/2024 hali iliyochangiwa na kuongezeka kwa uelewa wa wananchi pamoja na ubora wa huduma za uchunguzi zitolewazo na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia wa Serikali.
Hayo yameelezwa Machi 14, 2025 na Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kipindi cha miaka minne (4) ya Serikali ya Awamu wa Sita.
Dkt. Mafumiko amesema uchunguzi wa kisayansi wa kimaabara umekuwa na mchango mkubwa katika kusaidia kuchangia katika mnyororo wa haki jinai wa kutoa haki stahiki kwa mhusika na kwa wakati, masuala ya kijamii kama vile uhalali wa watoto kwa wazazi na matibabu kwa wagonjwa wanaohitaji huduma ya kusafishwa figo kwa kufanya uchunguzi wa sampuli za maji tiba yanayotumika pamoja na kupandikizwa figo ili kubainisha uhusiano uliopo kati ya mtoaji na mpokeaji wa figo kabla ya upandikizaji kufanyika.
“Ongezeko hili ni kutokana na ushirikiano na taasisi za Serikali za udhibiti kama vile Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Madawa ya Kulenya (DCEA), Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na wadau wa afya zikiwemo hospitali, OSHA (Usalama mahali pa kazi) na NEMC (Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira) na wadau wengine wanaotumia huduma za Mamlaka ili kupata uhakika wa ubora wa bidhaa zao,” ameeleza Dkt. Mafumiko.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Masuala ya Sayansi Jinai kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fedelis Bugoye ametaja idadi ya waliopima vinasaba nchini kwa mwaka 2024 hadi kufikia Disemba jumla ya majalada 524 yamechunguzwa.