Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

UBORA WA HUDUMA UZINGATIE LUGHA YA STAHA.

Posted on: March 26th, 2024



Na WAF-MWANZA

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. John Jingu amewataka wahudumu wa afya nchini kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi kwa kuzingatia lugha zenye staha na kutoa huduma stahiki kwa wagonjwa.

Dkt. Jingu ameyasema hayo wakati akiongea na watumishi wa sekta ya afya kwenye mkoa wa Mwanza baada ya kutembelea Hospitali ya Rufaa Mkoa huo Sekou Toure na Hospitali ya Kanda Bugando akiwa ameongozana na mganga mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu.

Dkt. Jingu amesema kazi ya utumishi wa afya ni kazi maalumu ambayo inalengwa kwa watu maalumu hivyo kila mtu awajibike kutekeleza kazi zake kwa ufanisi hali itakayowezesha kutaboresha huduma za Afya nchini

“Serikali imewekeza kwa asilimia kubwa katika sekta ya afya ikiwemo miundombinu, vifaa, vifaa tiba na dawa, hivi vyote havina tija kama hatutokua na huduma nzuri kwa wateja, hivyo tutumie lugha nzuri na yenye staha ikiwa ni Pamoja na kutoa huduma stahiki kwa wagonjwa”. Amesema Dkt. Jingu

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu amewaasa watumishi hao kuendelea kujali na kuthamini huduma bora kwa wananchi huku akiwatia moyo watumishi kuendelea kutoa huduma bora ndani ya jamii.

Prof. Nagu amewapongeza watumishi hao kwa juhudi kubwa ya kuwajali na kuwathamini wagonjwa kwani kazi ya kuwahudumia wagonjwa na Kazi maalum kwa watu maalum.

Akizungumza kwaniaba ya Watumishi Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa mkoa Sekou Toure Dkt. Bahati Msaki amemshukuru Katibu Mkuu wizara ya Afya Dkt. John Jingu Pamoja na Mganga mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu kwa kuwasihi na kuwapongeza watumishi hao Pamoja na kuahidi kuendelea kufanya kazi kwa juhudi ili kuboresha huduma za afya kwa jamii.