Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

TUTAENDELEA KUSHIRIKIANA NA WADAU KATIKA KUIMARISHA SEKTA YA AFYA NCHINI

Posted on: November 22nd, 2024

Na WAF - Dar es Salaam

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Jamhruri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zitaendelea kushirikiana na wadau pamoja na taasisi zote za afya ili kuhakikisha kuwa huduma za afya zinaimarika ikiwa ni pamoja na kukabiliana na dharura za kiafya.

Mhe. Majaliwa ametoa kauli hiyo Novemba 21, 2024 wakati wa hafla ya uzinduzi wa ripoti ya mapitio ya hali ya utekelezaji wa Afya kwa wote na utayari wa kukabiliana na dharura nchini lililofanyika katika hoteli ya Hyatt jijini Dar es Salaam.

Mhe. Waziri Mkuu amewashuruku wadau wote kwa ushirikiano wanaoutoa kwa Serikali zote mbili na kwamba zinathamini mchango wao na zitaendelea kuunga mkono katika yale ambayo wadau hao pia wanaunga mkono hasa katika mkakati wa Serikali wa utekelezaji wa afya kwa wote na utayari dhidi ya dharura.
“Ninatoa pongezi kwa timu ya wataalamu ambayo imefanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kuwa taarifa ya hali ya utekelezaji wa afya kwa wote pamoja na utayari dhini ya dharura inapatikana na kuwasilishwa kwa ajili ya kujadiliwa, nina imani itakwenda kuleta maslahi kwa nchi,” amesema Mhe. Majaliwa.

Amesema mjadala huu utarahisha utekelezaji wa vipaumbele vya afua zote muhimu katika utekelezaji wa shughuli za Serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya. Vilevile itakuwa fursa kwa wadau kuelewa maeneo yanayofanya vizuri na yale yenye changamoto ili Serikali iweze kuyapatia ufumbuzi.

Awali akizungumza katika hafla hilo Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewezeka kwa kiasi kikubwa katika sekta ya Afya kwani fedha zaidi ya Shilingi Trilioni 6.2 zimetumika katika kuimarisha sekta ya afya ndani ya miaka mitatu.

Amesema kutokana na uwekezaji huu Bima ya Afya kwa wote itakuwa ni muarobaini kwa kuhakikisha Watanzania wananufaika na uwekezaji huo kwa kupata huduma za afya wakiwemo walio na vipato duni kutokana na jitihada zinazofanywa na Serikali za kutenga fedha kwa ajili ya kundi hilo.