TUTAENDELEA KUSHIRIKIANA NA SEKTA BINAFSI KUHUDUMIA WANANCHI
Posted on: October 2nd, 2024
-Tunatambua mchango wa Sekta binafsi katika Sekta ya Afya.
Na WAF - Zanzibar
Serikali kupitia Wizara ya Afya imejipanga kuendelea kuwekeza katika Vifaa, Vifaa Tiba, Dawa pamoja na kutoa huduma kwa kushirikiana kwa karibu na Sekta Binafsi ili wananchi wapate huduma iliyo bora na salama.
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hayo leo Oktoba 1, 2024 katika ufunguzi wa mkutano wa 11 wa 'Tanzania Health Summit' ambapo mkutano huo umefunguliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla mjini magharibi unguja.
"Tunakila sababu ya kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kipindi kifupi Serikali imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika maeneo ya ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya kutolea huduma za Afya katika maeneo mbalimbali nchini hasa eneo la afya msingi, Hospitali za mikoa hadi Taifa." Amesema Waziri Mhagama
Aidha, katika kuendelea kuboresha miundombinu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa jumla ya shilingi trilioni 1.02 ambayo imesaidia kuwezesha kuongezeka kwa idadi ya vituo vya kutolea huduma za afya kutoka vituo elfu 8,549 mwaka 2021 hadi kufikia vituo 9,693 mwaka 2024 hii ni sawa na ongezeko la vituo 1,144.
"Vilevile Serikali ya awamu ya Sita imewekeza katika ununuzi na usimikaji wa Vifaa Tiba vya kisasa vya uchunguzi na ugunduzi wa magonjwa mbalimbali ikiwemo MRI 13 kutoka 7 mwaka 2021, CT-Scan 45 kutoka 12 mwaka 2021, Digital X-Ray 346 kutoka 147 mwaka 2021, Ultrasound 668 kutoka 476 mwaka 2021." Amesema Waziri Mhagama
"Serikali imeendelea kuimarisha huduma za dharura na huduma kwa wagonjwa mahututi ambapo hatua hii imewezesha kupatikana kwa huduma za kibingwa za uchunguzi kutoka katika ngazi ya Hospitali za Rufaa za Mikoa hadi Hospitali za Taifa." Amesisitiza Waziri Mhagama.
Katika ufunguzi huo Waziri Mhagama ameelekezea mafanikio ya utekelezaji wa mpango wa huduma za mkoba za madaktari bingwa na ubingwa bobezi ambao umeweza kufikia mikoa yote 26 na halmashauri 182 ambapo jumla ya wagonjwa Milioni 4,766,910 walipatiwa huduma hizo kwa kipindi cha kuishia Juni, 2024.