Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

TUSIISHI KINAJIMU, TWENDE KWA WATAALAM WA AFYA: WANANCHI SIMIYU

Posted on: June 21st, 2024



Na WAF, SIMIYU

Jamii mkoani Simiyu wameombwa kuacha kuishi kwa kubashiri juu ya afya zao na badala yake waende kwa wataalam wa afya kwa uchunguzi na matibabu.

Wakiongea kwenye kambi maalum ya Madaktari Bingwa ya robo mwaka ya mwisho kwa mkoa huo, Juni 20, 2024 katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wamesema baadhi ya wanajamii hawajitokezi haraka kwa wataalam kutokana na kubashiri kile wanacho umwa.

"Kwa muda wa miaka minne mwanangu amekuwa na changamoto ya upumuaji, lakini mimi nilikuwa nadhani anasumbuliwa na tonsesi nilipo wanna wataalama wakasema ni nyama za puani" amesema Bi. Ester Charles

Kwa upande wake Bwana Zacharia Jilala, yeye amesema amedumu na tatizo la kuziba nta kwenye masikio kwa zaidi ya mwaka mmoja huku akitumia dawa bila vipimo vya matabibu stahiki.

Kufuatia hali hiyo wananchi hao wote kwa pamoja, wametoa wito kwa wanajamii wengine kuharakisha kuwaona wataalam wapatapo changamoto ya kiafya.

Wakati huo huo imebainika kuwa wananchi wengi mkoani Simiyu wamekuwa na matatizo ya Masikio, Koo na Pua hali inayo isukuma Hospitali ya Rufaa ya mkoa kuanza kufanya tafiti.

Akizungumza Hospitalini hapo Dkt. Juma Muna, mratibu wa tiba wa Hospitalini hiyo amesema wapo mbioni kufanya utafiti ili kubaini tatizo ni nini.

"Hii ni mara ya pili, tunafanya Kambi ya Madaktari Bingwa lakini tulicho baini ni watoto wengi kuwa nyama za puani hivyo tunataka kuwekeza katika tafiti ili tuweze kubaini chanzo" amesema Dkt. Muna

"Kwa kuwa waathirika wengi ni watoto tunataka kujua, Je! tatizo hutokea wakati upi je niwakati wa ujauzito, kujifungua au ni ulaji wa vyakula? amhiji Dkt. Muna.”

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Masikio, Pua na Koo, Richard Shija amesema zaidi ya wananchi 150 walijitokeza kwa ajili ya kuchunguzwa magonjwa Pua, Koo na Masikio ambapo kati yao 24 walilazimika kufanyiwa upasuaji.

Akitoa tathmini ya jumla mratibu wa huduma za mkoba kutoka Wizara ya Afya, Dkt. John Mombeki, amesema Hospital ya Rufaa ya wa Simiyu imeendelea kutekeleza Sera ya Afya inayo himiza utoaji wa Huduma za Kibingwa kila robo Mwaka kwa kila hospitali ya mkoa.

MWISHO