Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

TUNZENI HOSPITALI KWA MASLAHI YA UMMA KUPATA HUDUMA

Posted on: August 2nd, 2024

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wa Hospitali ya Wilaya ya Gairo Mkoani Morogoro pamoja na wananchi kuitunza na kuisimamia vizuri Hospitali ya Wilaya hiyo ili iendelee kutoa huduma kwa wananchi. 


Rais Samia amesema hayo leo Agosti 2, 2024 baada ya kuzindua Hospitali ya Wilaya ya Gairo mkoani Morogoro itakayotoa huduma za Afya ikiwemo huduma ya uzazi mama na mtoto kutokana na kuwa na vifaa vya kisasa vya kutosha. 

Amesema, ameridhishwa na matumizi ya fedha alizozitoa kwa kazi ya kujenga Hospitali ya Wilaya ya Gairo ambayo inavifaa vya kisasa ambapo amewataka wananchi waitunze ili iendelee kutoa huduma za Afya. 


"Serikali imejidhatiti kuleta maendelea kwa wanachi, tuendelee kudumisha amani iliyopo, tuendelee kuzalisha mazao ya biashara ikiwemo mahindi, maharage, mbaazi kwa kuwa soko lipo, muendelee kuiunga mkono serikali yenu ili iendelee kuleta maendeleo kwenu"

Kando ya ziara hiyo akiongea na waandishi wa habari Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema Hospitali hiyo ni moja kati ya kazi nzuri za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kusogeza huduma za Afya karibu zaidi na wananchi. 


Amesema, Hospitali hiyo imekamilika kwa kiasi kikubwa na ina vifaa vya kisasa ambapo huduma za upasuaji wa kina mama inapatikana katika Hospitali hiyo inayowezesha watu kupata huduma hizo za uchunguzi wa magonjwa, upasuaji, X-Ray pamoja na Dawa kwa karibu. 

"Awali tulikua na kituo cha Afya ambacho kilikua hakina miundombinu ya kutosha, hivyo kuzinduliwa kwa Hospitali hii kutasaidia wananchi kupata huduma kwa karibu bila kwenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro wala Dodoma", amesema Waziri Ummy  


Kuhusu Dawa, Waziri Ummy amesema bajeti ya dawa kwa Mwaka 2021 Wilya ya Gairo ilikua ni Milioni 375, Rais Samia ameongeza hadi kufikia Milioni 509 hali ambayo itachochea kupatikaa kwa bidhaa hizo za dawa. 


Mwisho, Waziri Ummy amesema changamoto wanayopambana nayo kama Serikali na Wizara ya Afya ni ugharamiaji wa huduma za Afya kwa kuwa watanzania walio wengi hawajajiunga na Mfuko wa Bima ya Afya.


Rais Samia yupo Mkoani Morogoro kwa ziara ya siku Saba ambapo atakagua miradi yote iliyotolewa fedha na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.