Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

TUNAFANYA MAPITIO YA VIGEZO VYA POLYCLINICS, NYINGI NI VICHOCHORO VYA WIZI DHIDI YA NHIF; WAZIRI UMMY MWALIMU

Posted on: July 8th, 2022

Serikali imesema haikusudii kufuta Kliniki za Kibingwa (Polyclinics) zilizopo nchini bali inapitia vigezo vya kuwa na Polyclinics ambazo hivi karibuni zimeibuka kliniki nyingi ambazo zimekuwa ni vichochoro vya udanganyifu dhidi ya Mfuko wa Taifa wa NHIF.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu leo alipokutana na Watoa Huduma za Afya wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya wa Mkoa wa Dar Es Salaam.

"Hatufuti wala hatukusudii kufuta Polyclinics, lakini tunafanya mapitio ya vigezo vya Polyclinics kwasababu ndio kichochoro kingine cha udanganyifu dhidi ya NHIF na ndio maana kuna wingi wa Kliniki za Kibingwa zinazoanzishwa amabzo hazina vigezo kwa sababu ya kufanya udanganyifu” amesema Waziri Ummy Mwalimu.
Amesema Sera ya Afya inataka Serikali kuendelea kutambua mchango wa Sekta binafsi kwa kusaidia kutoa huduma za afya nchini na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri na wezeshi kwa sekta binafsi kuweza kufanya kazi kwa sababu Serikali peke yake haiwezi.

“Tunafungua hizi kliniki kwa ajili ya NHIF au kwa ajili ya Watanzania? Tunataka kuondoa ujanja ujanja, NHIF ina wanachama Milioni 4.6 kuna Watanzania wengi bado hawana Bima ya Afya, nao wahajitaji pia kuhudumiwa, kwa hiyo lengo la kwanza kufungua kituo cha kutolea huduma za afya kiwe ni kuhudumia Watanzania” amesema Waziri Ummy.

Waziri ummy amesema wamebaini tabia ya wataalam ambao wanafanya kazi kwenye kliniki binafsi mara baada ya kutoka kazini ambapo wataalam hao huchukua vipimo kutoka kwa mgonjwa na kurudi kufanyia uchunguzi kwenye vituo vya umma na mwisho wa siku wao ndio wanufaika wakubwa kutoka NHIF huku wakiwa wametumia vifaatiba vya Hospitali ya Umma kwa udanganyifu na maslahi binafsi.
“Tunataka Polyclinics hizi ziendelee kuwepo na kutoa huduma kwa wananchini na hadi kufikia mwezi Machi 2022 kulikuwa na jumla ya Kliniki za Kibingwa 299 sawa na asilimia 3.3 ya vituo vyote vya kutolea huduma” amesema Waziri Ummy.
Waziri Ummy amesema hadi kufikia Mwezi Mei 2022 Vituo vya kutolea huduma za afya nchini ambavyo vimesajiliwa na Serikali vilikuwa 8549 huku vinavyomilikiwa na Serikali vikiwa ni 6377 huku vya binafsi vikiwa 2172 na kuongezea kuwa Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi ya Sekta binafsi kuchangia katika Huduma za Afya nchini.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Bw. Benard Konga amesema hadi kufikia Mwezi Machi NHIF ilikuwa na jumla wanachama Milioni 4.63 ambao wanahudumiwa katika vituo vya umma na binafsi vya kutolea huduma za afya nchini.

Amesema hadi kufikia Mwezi Machi 2022 NHIF ilikuwa na jumla ya vituo 8883 vya umma na binafsi ambavyo vinatoa huduma kwa wanachama wa NHIF nchi nzima ambapo kati ya vituo hivyo 299 ni Kliniki za Kibingwa.

Mkurugenzi Konga amesema hadi kufikia Mwezi Machi NHIF ililipa jumla ya Shilingi Bilioni 382.1 ambazo kati ya fedha hizo asilimia 42 ililipwa kwa watoa huduma Sekta Binafsi, asilimia 28 kwa vituo vya kutolea huduma za afya vinavyomilikwa na Taasisi za Dini huku asilimia 30 ikilipwa kwa vituo vya Serikali.