Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

TUMIENI FURSA YA UJIO WA MADAKTARI BINGWA KWENDA KUPATA HUDUMA ZA AFYA

Posted on: May 14th, 2024Na WAF – Dodoma

Wananchi wa Mkoa wa Dodoma atakiwa kutumia vizuri fursa ya ujio wa madaktari bingwa kwenda kupata huduma za ubingwa na ubingwa bobezi katika hospitali za wilaya zote mkoani humo kwa muda wa siku saba wa uwepo wa madaktari hao.

Hayo yamesema na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule tarehe 15 Mei, 2024 wakati akiwapokea Madaktari Bingwa wa Rais Samia baada ya kuwasili mkoani Dodoma kwa ajili ya kuwahudumia wananchi katika hospitali za halmashauri saba zilizopo mkoa wa humo.

Mhe. Rosemary amewaasa madaktari bingwa kwenda kufanya kazi kwa kujituma zaidi na kuzingatia maadili ili kutimiza lengo la Mhe. Rais na Wizara ya Afya kwa wananchi.

“Sisi kama mkoa tumejipanga kuhakikisha wananchi wanapata huduma nzuri kama alivyokusudia Mhe. Rais kuona wananchi wanasogezewa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi karibu zaidi. Wapo watu wengi huku mikoani ambao wanaweza wakapewa rufaa ya hospitali ya mbali, lakini tunajua baadhi ya Watanzania hali zao ni za chini hata usafiri ni shida hivyo kuwafuata walipo kutawasaidia kunufaika na huduma hizi”. Amesema Mhe. Senyamule

Mhe. Rosemary ametoa wito kwa Watanzania kujitokeza katika hospitali za wilaya zote mkoani Dodoma, ili kunufaika na ujio huu wa madaktari bingwa mpango huo ambao umenuia kusogeza huduma za ubingwa na Ubingwa bobezi karibu na wananchi, pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wa mbalimbali katika ngazi ya afya ya msingi.

Miongoni mwa huduma za kibingwa watakazonufaika nazo wananchi wa Mkoa wa Dodoma kwa siku tano, kuanzia Mei 13 hadi 17, ni pamoja na uwepo wa wataalamu wa huduma za ganzi na usingizi, magonjwa ya ndani, huduma za kibingwa za upasuaji, huduma za kibingwa za watoto na magonjwa ya wanawake na uzazi.

Mwisho.