TUMERIDHISHWA NA HUDUMA ZA AFYA KATIKA HOSPITALI YA RUFAA IRINGA
Posted on: August 6th, 2024
Na WAF, Iringa
Kamati ya Kudumu ya Afya na Masuala ya Ukimwi inayoongozwa na Kaimu Mwenyekiti, Christine Mnzava, akiambatana na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel na wajumbe wake, imefanya ziara katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa kwa ajili ya kuangalia hali ya utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.
Ziara hiyo imefanyika leo Agosti 06, 2024 katika mkoa wa Iringa ambapo Mhe. Mnzava ameipongeza hospitali hiyo kwa jitihada kubwa za kuboresha huduma za afya na kutoa huduma bora wakati wote.
Aidha, ameeleza kuridhishwa kwake na maendeleo yaliyopatikana na juhudi zinazofanywa na watumishi wa hospitali katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya.
“Nawapongeza kwa juhudi zenu za dhati katika kuboresha huduma za afya. Huduma zenu zimeendelea kuwa bora na zenye viwango vinavyokidhi mahitaji ya wananchi wetu,” amesema Mhe. Mnzava.
Aidha, amewataka watumishi wa hospitali hiyo kuendelea kuishi katika miiko ya kazi na kujitoa kwa ufanisi katika utendaji wao wa kazi. Ameeleza kuwa nidhamu na kujituma ni nguzo muhimu katika kufanikisha utoaji wa huduma bora za afya.
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, ameongeza kuwa Serikali itaendelea kutoa msaada na rasilimali muhimu ili kuhakikisha huduma za afya zinaendelea kuboreka katika hospitali hiyo na maeneo mengine nchini.
Ziara hiyo imetoa fursa kwa wajumbe wa kamati kujionea hali halisi ya utoaji wa huduma za afya na kupokea taarifa za huduma za hospitali hiyo.