Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

TUMEIMARISHA UTEKELEZAJI WA AFUA ZA AFYA, MAZINGIRA

Posted on: March 16th, 2025

NA WAF - Kilimanjaro

Mkuu wa Wilaya ya Siha, Mhe. Dkt. Christopher Timbuka, amesema Wilaya ya Siha imeimarisha utekelezaji wa afua za afya na mazingira unaojumuisha ujenzi na matumizi sahihi ya vyoo bora, lishe, hedhi salama, usafi wa mazingira na mazoezi.

Dkt. Timbuka ameyasema hayo leo, Machi 15, 2025, wakati timu ya Wizara ya Afya kupitia kampeni ya Mtu ni Afya ilipofika ofisini kwake kujitambulisha, wakiambatana na Balozi wa kampeni hiyo, Mrisho Mpoto, pamoja na mzabuni wa Project Clear.

Mhe. Dkt. Timbuka amesema Wilaya ya Siha imejiandaa na itashiriki kikamilifu katika kampeni ya Mtu ni Afya, inayolenga kuwalinda wananchi dhidi ya magonjwa ya kuambukiza.

“Tayari Wilaya ya Siha imefikia asilimia 91.2 ya wananchi waliojenga na kutumia vyoo bora, na tunaendelea kuwahamasisha wananchi ambao hawana vyoo bora ili kufikia mwaka 2026 wananchi wote wawe na vyoo bora na kuvihifadhi vizuri,” amesema Mhe. Dkt. Timbuka.

Aidha, Dkt. Timbuka amesema hali ya udumavu kwa watoto katika Wilaya ya Siha imefikia asilimia 18.9, huku lengo likiwa ni kupunguza hadi asilimia 18 ifikapo mwaka 2026.

Kwa upande wake, Balozi wa Kampeni ya Mtu ni Afya Awamu ya Pili, Mrisho Mpoto, amesema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI, baada ya kuboresha miundombinu ya afya, sasa inajikita katika kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu kujikinga na magonjwa.

Kampeni ya Mtu ni Afya Awamu ya Pili ilizinduliwa na Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango, tarehe 09 Mei 2024, kwa lengo la kuhamasisha wananchi kujikinga dhidi ya magonjwa ya kuambukiza kupitia usafi na lishe bora.

Kampeni hii inaongozwa na kaulimbiu inayosema “Mtu ni Afya, Fanya Kweli, Usibaki Nyuma.”