Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

TUJITOKEZE KUCHANJA CHANJO YA UVIKO-19 ILI TUPATE KINGA YA JAMII; WAZIRI UMMY MWALIMU

Posted on: July 7th, 2022


Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu ametoa rai kwa wananchi kuchanja chanjo dhidi ya UVIKO-19 ili Tanzania iwe na watu wengi waliochanja na kupata Kinga ya Jamii dhidi ya UVIKO-19.

Waziri Ummy Mwalimu amesema hayo leo Jijini Dar Es Salaam mara baada ya kutembelea Maonyesho ya Kimataifa ya 46 ya Biashara ya Saba Saba akiwa pamoja na Mratibu wa Kimataifa wa Mapambano dhidi ya UVIKO-19 kutoka umoja wa Mataifa Dkt Ted Chaiban ambapo walitoa elimu na hamasa ya chanjo dhidi ya UVIKO-19 kwa wananchi.

“Chanjo dhidi ya UVIKO-19 ni salama na haina madhara na ili tuweze kupata kinga dhidi ya Ugonjwa huu wa UVIKO-19 ni lazima tuchanje” amesema Waziri Ummy Mwalimu.

Waziri Ummy amesema kwamba ili Duniani tuweze kuwa na Kinga ya Jamii na kuudhibiti ugonjwa wa UVIKO-19 inatubidi angalau asilimia 70 ya watu Duniani tuwe tumechanja hivyo basi Tanzania nasi tunawajibika kuhakikisha tunafikia lengo la Dunia na kuwa asilimia 70 ya Watanzania wenye umri wa miaka 18 ambao wamechanja.

Waziri Ummy amesema Wazee walio na umri wa zaidi ya miaka 60 pamoja na watu wenye magonjwa yasiyoambukiza wako hatarini kuugua ugonjwa wa UVIKO-19 hivyo ni vyema wajitokeze kupata chanjo dhidi ya UVIKO-19 huku akihimiza Vijana kupata chanjo ili tuweze kupata kinga ya jamii.

Waziri Ummy amesema Wizara inatumia mbinu mbalimbali za kuelimisha na kuhamasisha jamii kujitokeza kupata chanjo huku akitumia fursa hiyo kumpongeza Bi. Zamaradi Mketema kwa kuja na wazo la kuwaweka Wasanii sehemu moja na kutoa elimu ya Chanjo ya UVIKO-19 katika Maonyesho ya Saba Saba.

“Wasanii wana wafuasi wengi hadi kwenye mitandao na tumeona wazo la Zamaradi limelipa, ndani ya siku 6 zaidi ya watu 2,000 wamechanja” Amesema Waziri Ummy Mwalimu.

Kwa upande wake Mratibu wa Kimataifa wa Mapambano dhidi ya UVIKO-19 kutoka umoja wa Mataifa Dkt Ted Chaiban ameipongeza Tanzania kwa kuendeleza mapambano dhidi ya UVIKO-19 na kuweza kuongeza kiwango cha watu waliochanja kutoka asilimia 6.8 hadi kufikia asilimia 12.6 hadi sasa.

Dkt. Ted Chaiban amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuongoza mapambano dhidi ya UVIKO-19, Viongozi wa Wizara pamoja na wadau akiwemo Bi. Zamaradi Mketema kwa kuja na wazo zuri la kuchanja maelfu ya watu katika Maonyesho ya Saba Saba.

“Kuchanja chanjo ya UVIKO-19 kunakupa kinga dhidi ya ugonjwa huo, chanjo inalinda familia yako pamoja na jamii, sisi kama wadau wa maendeleo tuko hapa kusaidia Serikali kuhakikisha inafikia lengo la uchanjaji wa asilimia 70 ili kuwa na Kinga ya Jamii” amesema Dkt. Chaiban.

Mwsho.