TIBA ASILI ZATAKIWA KUTHIBITISHWA USALAMA ILI KUSAIDIA TIBA KWA WANANCHI
Posted on: August 29th, 2025
Na WAF, Dodoma
Wataalam wa afya wametakiwa kuweka jitihada kulinda usalama, ufanisi na ubora kwenye tiba asili ili kuepusha madhara kwa watumiaji ikiwemo kuunda mifumo ya ushirikiano pamoja na rufaa kati ya matibabu kwa kutumia tiba asili na madaktari wa kiafya.
Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto Dkt. Ahmad Makuwani ambaye amemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt.Seif Shekhalage kwenye ufunguzi wa kongamano la Wiki ya Tiba Asili leo Agosti 29, 2025 Jijini Dodoma amesema tiba asili zinaweza kuingia kwenye soko kwa kutoa tiba ambazo zitanufaisha watu wengi ikiwa zina usalama na ubora unaofaa kwa matumizi ya wananchi.
Makuwani amebainisha kuwa Tanzania inatoa huduma jumuishi kwa hospitali za rufaa za mikoa 14 na takriban ni dawa 26 zinapatikana katika huduma hizo na ujumuishaji huo utahakikisha wagonjwa wanapata faida kubwa kwa mifumo yote ikiwemo ya kisasa na ile ya asili.
“Nimewatolea mfano dawa ambazo zilitumika wakati wa UVIKO 19 au dawa ambayo imeasisiwa kule Sokoine, kama tutaziwekea usalama na ubora unaotakiwa zitakuwa ni miongoni mwa tiba nzuri zitakazosaidia wananchi,” amesema Dkt. Makuwani.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu Prof. Said Shebe Aboud amesema lengo la kukutanishwa wanasayansi kwenye Wiki ya Tiba Asili ni kuwa na majadiliano yatakayoleta maazimio ya kuendeleza tiba asili ndiyo maana Serikali imeidhinisha huduma jumuishi kwemo kwenye hospitali za rufaa.
“Ni kujadiliana lakini mwisho wa siku kuja na maadhimio ambayo yatasababisha au yatapelekea tasnia ya tiba asili kuendelea kuboreka zaidi na tayari kuna huduma jumuishi yani tiba asili zinatolewa kwenye hospitali za rufaa na hii inasaidia mgonjwa anapokwenda hosptirali anachagua aina ya huduma ya matibabu yake,” amesema Prof. Shebe.
Dhima kuu ya kongamano la mwaka huu yanye kaulimbiu ya ‘’tuimarishe huduma za tiba asili zenye ushahidi wa kisayansi’’ ni kuboresha tiba asili kwa usawa wa afya, ubunifu na maendeleo endelevu inayobeba maono ya muda mrefu.