TEHAMA KUCHOCHEA MAGEUZI UTOAJI HUDUMA SEKTA YA AFYA
Posted on: January 16th, 2026Na WAF, Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya afya imefanya marekebisho ya mifumo ya TEHAM ili kurahisisha na kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima wakati wa upatikanaji wa huduma kwenye hospitali nchini ikiwa na shabaha ya kurahisha huduma pamoja na kuokoa muda wa mwananchi kuhudumiwa.
Hayo yamebainishwa Januari 16, 2026 na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Florence Samizi mbele ya kamati ya kudumu ya ya Bunge ya Afya na masuala ya UKIMWI Bungeni jijini Dodoma kwaniaba ya Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa.
Samizi amesema, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia mabadiliko hayo ya mifumo ambayo itakuwa rahisi kusomana na kujua maendeleo ya mgonjwa kwa urahisi popote atakapopata huduma ikiwepo kuhama kutoka ngazi moja kwenda nyingine kutegemea na rufaa aliyopewa.
"Mmemsikia Mhe. Waziri kwamba anataka mdumo wa 'end to end health insurance', mfumo ambao utafuatilia safari ya mgonjwa, kuanzia anapoingia kwenye geti mpaka anapotoka na utadhibiti matumizi ambayo sio ya lazima na Mhe. Rais ameridhia mabadiliko hayo ya mfumo" - amesema Dkt. Samizi
Marekebisho ya mifumo ya TEHAMA katika sekta ya afya ni nyenzo muhimu kwa Serikali kuimarisha utoaji wa huduma bora, uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za umma, sambamba na mkakati wa Taifa wa mageuzi ya sekta ya afya unaolenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki kwa wakati, kwa gharama nafuu na kwa ufanisi zaidi katika hospitali zote nchini.