TANZANIA YAPOKEA NCHI 14 KUJIFUNZA KUPUNGUZA VIFO VYA MAMA NA MTOTO
Posted on: December 6th, 2024Na WAF, Dodoma
Serikali ya Tanzania imepokea ugeni wa wajumbe kutoka nchi 14 ukiongizwa na Shirika la kuthibiti magonjwa Afrika (CDC Afrika) kwa lengo la kujifunza namna Serikali ya Tanzania ilivyopiga hatua kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi na watoto wachanga.
Wajumbe hao wamefanya ziara katika kituo cha Afya cha Soya kilichopo Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma Desemba 5, 2024 wakiongozwa na watendaji kutoka Wizara ya Afya Idara ya huduma za Afya ya uzazi, mama na mtoto.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo Mkuu wa Progamu ya Uzazi Salama Wizara ya Afya Dkt. Phineas Sospeter amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi chache barani Afrika zilizoweza kupunguza vifo vya wajawazito kwa kiasi kikubwa ambapo toka miaka saba iliyopita vifo vya vitokanavyo na uzazi vimepungua kutoka 556 kwa kila vizazi hai 100,000 kwa mwaka 2015/2016 na kufikia vifo 104 kwa kila vizazi hai laki moja mwaka 2022.
“Hizi nchi kumi na nne zimekuja kujifunza namna tunavyotekeleza afua mbalimbali, wameweza kujifunza namna mifumo ya afya inavyofanya kazi kutoka ngazi ya taifa hadi chini kwenye Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, na kuona namna utashi wa kisasa ulivyochangia kwa kiasi kikubwa katika kupunguza vifo hivyo,” amesema Dkt. Sospeter
Naye Mganga mfawidhi kituo cha afya cha Soya Dkt. Sabuni Kasongi amesema jumla ya wakina mama 83 wamepatiwa huduma za kujifungua kwa njia ya upasuaji wa dharura tangu kuanzishwa kwa huduma hiyo mwezi Oktoba 2023 katika kituo cha Afya cha Soya kilichopo Halmashauri ya wilaya ya Chemba.
“Wajawazito na watoto wachanga wenye changamoto mbalimbali zinazowalazimu kupewa rufaa tunawapeleka hospitali ya wilaya ya Chemba na ya mkoa wa Dodoma kwa kutumia usafiri wa m-mama au ambulance. Kwa upande wa wa m-mama jumla ya watoto waliofaidika na huduma hiyo ni 22 na wajawazito 72 tangu mfumo huo ulipoanza mwaka 2022,” ameeleza Dkt. Kasongi.
Wajumbe hao ni kutoka nchi ya Ethiopia, Gambia, Lesotho, Eswatini, DRC Congo, Chad, Nigeria, Somalia Guniea, Kenya, Uganda, Zambia, Egypt na South Sudan.