Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

TANZANIA YAJIDHATITI KATIKA MATUMIZI YA TEHAMA KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA

Posted on: May 19th, 2025

Na WAF - Geneva, Uswisi

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejidhatiti kikamilifu katika matumizi ya TEHAMA kama kichocheo muhimu cha huduma za afya ya msingi na Afya kwa wote ikiwa ni pamoja na mfumo wa taarifa za Afya za Wilaya (DHIS2) ambao unatumika nchi nzima kufuatilia taarifa za afya kwa wakati.

Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe amesema hayo leo Mei 19, 2025 kwenye Mkutano wa pembezoni uliokuwa na lengo la kubadilishana uzoefu katika matumizi ya TEHAMA kwenye kuboresha utoaji wa huduma za Afya ya unaoendelea Geneva nchini Uswisi, Mkutano huo uliongozwa na Dkt. Margaret Chan aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani na kushirikisha nchi za Tanzania, China, Peru, Ethiopia na Thailand.

"Sehemu nyingine tuliyofanikiwa kama nchi ni kuimarisha mfumo wa taarifa za Rasilimali Watu wa Afya ambao husaidia kugawa wafanyakazi wa afya kwa uwiano, kuimeimarisha upatikanaji wa dawa muhimu hadi ngazi ya jamii pamoja na ubunifu wa mfumo wa uhudumiaji wa haraka kwa wajawaziro (M-Mama)," amesema Dkt. Magembe

Dkt. Magembe ameongeza kuwa ili kuendelea kutatua changamoto za Sekta ya Afya, Serikali imejipanga kuwekeza katika miundombinu ya kidigitali ya afya vijijini, kukuza uelewa na ujuzi wa kidigitali kwa watumishi, kuimarisha usimamizi wa taarifa, faragha, na matumizi ya maadili ya takwimu.