Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

TANZANIA NI SALAMA, KAGERA NI SALAMA HAKUNA TENA UGONJWA WA MARBURG

Posted on: June 2nd, 2023

Na WAF- Bukoba Kagera.

Waziri wa Afya Mhe @ummymwalimu ameutarifu umma wa Watanzania na Ulimwengu kwa ujumla kuwa Tanzania imeweza kupambana na kudhibiti ugonjwa wa Marburg na hivi sasa kuwa Mkoa huo na nchi kwa ujumla ni salama na hakuna maambukizi ya ugonjwa huo.

Waziri Ummy amesema hayo leo kwenye kwenye kilele cha mapambano dhidi ya ugonjwa wa Marburg ambao uliripotiwa kuingia nchini mnamo Machi 16, 2023, Kagera Tanzania.

“Leo Mwenyezi Mungu ametuwezesha, zimetimia zaidi ya siku 42 toka mgonjwa wa mwisho kupona Marburg, Kwa maana hiyo tumekidhi vigezo vya Shirika la Afya Duniani vya kutangaza mwisho wa ugonjwa wa Marbung, hivyo natangaza kwamba leo 02/06/2023 mlipuko wa ugonjwa wa Marburg tumeumaliza rasmi Mkoa wa Kagera” amesema Waziri Ummy Mwalimu.

Waziri Ummy amesema kuwa jitihada za pamoja za Serikali kwa kushirikiana karibu na Wadau wa maendeleo wa Sekta ya Afya na wa Kimataifa wamefanikisha mapambano hayo na kuweza kutangaza kutokomeza ugonjwa wa Marburg nchini ndani ya kipindi kifupi.

“Ni Fahari kwetu sisi Tanzania kwamba tumeweza kulinda Watanzania, tumeweza kutimiza wajibu wetu wa kimataifa wa kuilinda Dunia dhidi ya ugonjwa wa Marburg, nalishukuru sana Shirika la Afya Duniani kwa hapa Tanzania kwa kuongoza wadau wa kimataifa katika mapambano hayo” ameshukuru Waziri Ummy.

Amesema kuwa mafanikio hayo ya kudhibiti ugonjwa wa Marburg ni juhudi za pamoja za Serikali kuanzia ngazi ya Taifa hadi jamii kwa kushirikiana na wadau wote. Hivyo, ninawashukuru wataalamu wote wa afya Pia, natoa pongezi kwa viongozi wa kisekta na Watumishi wa sekta ya Afya kutoka Wizara ya Afya, OR-TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Taasisi za elimu nchini, Wananchi, wanahabari, sekta binafsi na wadau mbalimbali walioshirikiana nasi kwa hali na mali katika kukabiliana na ugonjwa huu.

"Niendelee kuwaomba Wananchi nkuwa macho wakati wote na endapo kutatokea tetesi za mhisiwa au mtu mwenye dalili za ugonjwa wowote usio wa kawaida au unaotia mashaka ni vyema kutoa taarifa sehemu husika" amesema Waziri Ummy.

#MtuniAfya #AfyaniMtaji