TANZANIA KUIMARISHA MIKAKATI YA MATIBABU YA SARATANI
Posted on: September 19th, 2025
Na WAF – Vienna, Austria
Serikali ya Tanzania inaendelea kupiga hatua muhimu katika uimarishaji wa huduma za saratani nchini kwa kuingia kwenye majadiliano na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA), lengo kuu likiwa ni kuboresha miundombinu na kuongeza uwezo wa wataalam wa ndani kutumia teknolojia za kisasa za nyuklia katika tiba ya saratani.
Hilo limejidhihirisha wakati wa Mkutano wa 69 wa Nishati ya Atomiki Duniani unaoendelea Viena, Austria ulioanza Septemba 15 na kutarajiwa kuhitimishwa Septemba 19, 2025 ambapo Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo unaongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Caroline Nombo.
Aidha Balozi wa Tanzania mjini Vienna, Mhe. Naimi Aziz, na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Dkt. Diwani Msemo wanashiriki katika mkutano huo pamoja na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomic (IAEA), Prof.Caroline Nombo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kujadili uimarishaji wa miundombinu ya matibabu ya saratani nchini.
Kupitia mkutano huo, Tanzania inatarajiwa kunufaika kwa kupewa mwongozo na msaada wa kitaalam utakaowezesha huduma za saratani zenye ubora wa kimataifa kupatikana ndani ya nchi. Hatua hii itapunguza kwa kiasi kikubwa mzigo wa kifedha kwa familia ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikilazimika kutafuta tiba nje ya nchi, sambamba na kuokoa muda wa wagonjwa kupata matibabu kwa haraka zaidi.
Miongoni mwa matokeo chanya ya Mkutano huo yanayotarajiwa ni kupata suluhu ya huduma za kisasa na zenye ubora wa kimataifa ndani ya nchi, bila kulazimika wagonjwa kusafiri kwenda nje kutafuta matibabu ya saratani hatua ambayo itazidi kupunguza gharama kubwa ambazo familia nyingi zimekuwa zikizibeba, sambamba na kuokoa muda wa wagonjwa kupata matibabu kwa haraka zaidi.
Aidha, kupitia mafunzo na ushirikiano utakaotokana na mkutano huo, wataalam wa Tanzania watajengewa uwezo mkubwa wa kutumia teknolojia ya nyuklia katika kutibu saratani, jambo linaloongeza ufanisi na kupunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali za rufaa.