Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

TANZANIA KUENDELEA KUIMARISHA AFYA MIPAKANI

Posted on: October 5th, 2025

Na WAF - Morogoro

Serikali kupitia Wizara ya Afya Idara ya Kinga kitengo cha Afya Mazingira na Usafi, Huduma za Afya Mipakani inaendelea kuimarisha afya mipakani katika kujikinga na magonjwa ya mlipuko ambayo yanaweza kujitokeza ndani na nje ya nchi.

Mkuu wa Kitengo cha Afya Mipakani kutoka Wizara ya Afya Dkt. Amour Seleman amesema hayo leo Oktoba 04, 2025 mkoani Morogoro kwenye kikao kazi chenye lengo la kufanya tathmini ya utekelezaji wa kazi za afya mipakani kwa kipindi cha mwaka 2024/25.

"Katika kutekeleza afua hizo leo tumekutana na wafawidhi wa afya mipakani ili kuendelea kujengeana uwezo na kuandaa mipango yetu ya utekelezaji na kutathmini utekellezaji uliopita kwa sababu kuna uwezekano mkubwa wa kusambaa kwa magonjwa kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine ikiwemo Tanzania," amesema Dkt. Seleman.

Amesema, hadi sasa Tanzania ina mipaka 59 ambayo ina watumishi wanaofanya kazi kwa saa 24 ambapo lengo la Wizara ni kutambua changamoto yoyote kwa haraka, watumishi pamoja na vifaa kinga vipo ili kujikinga na maambukizi ya magonjwa ya mlipuko.

Aidha, Dkt. Seleman ametoa wito kwa jamii kuendelea kuchukua hatua za kujikinga na magonjwa ya mlipuko ikiwemo kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni mara kwa mara na kutoa ushirikiano kwa watumishi wa afya mipakani pindi wanapotaka kutekeleza majukumu yao ikiwemo ya upimaji afya.

"Nitoe wito kwa jamii kuendelea kuchukua tahadhari katika kujikinga na magonjwa ya mlipuko ikiwemo kunawa mikono mara kwa mara, tunashukuru kuna vifaa vya kutosha mipakani ikiwemo vifaa vya kunawia mikono, lakini pia naomba tuwape ushirikiano wataalam wetu pindi wanapotoa huduma," amesema Dkt. Seleman.

Kikao kazi hicho kilichoanza mapema wiki hii kina lengo la kuboresha huduma za afya nchini na kinawahusisha wafawidhi wa vituo vya afya mipakani wapatao 59 pamoja na wataalam kutoka Wizara ya Afya makao makuu Dodoma.