Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

TANZANIA KUENDELEA KUDHIBITI MAGONJWA YALIYOKUWA HAYAPEWI KIPAUMBELE

Posted on: August 25th, 2022


Na. WAF - Dar es Salaam

Wizara ya Afya imeendelea na mpango mkakati wa kusambaza kingatiba kwa wananchi wote ili kudhibiti magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele ikiwemo matende na mabusha, vikope, kichocho, minyoo na Usubi ambapo hadi kufikia sasa Wilaya 9 zimebaki kutokomezwa kabisa kwa upande wa ugonjwa wa matende na mabusha.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 10 wa kutengeneza mpango kazi wa mwaka 2022/23 wa Mpango wa Taifa wa kudhibiti magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele, leo (Agosti 25, 2022) kwa Niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Mkurugenzi Mkuu NIMR Prof. Yunus Mgaya amesema lengo kuu la mpango huo ni kutokomeza kabisa magonjwa hayo kule ambako yanaendelea kutokea.

"Tumeweka nguvu kubwa kabisa katika kuhakikisha kwamba maeneo yote ambayo yameathirika na magonjwa haya, wananchi wanapewa kingatiba kwa ujumla"

Aidha, Prof. Mgaya amesema mpaka kufikia mwaka 2030 wataweza kutokomeza magonjwa kwa kiasi cha kutangaza kwamba magonjwa hayo siyo tena mzigo katika sekta wa Afya nchini Tanzania.

"Mkakati wa kutoa kingatiba umewezesha kupunguza magonjwa katika sehemu mbalimbali za nchi, wilaya nyingi ambazo zilikuwa na matatizo haya sasa hivi hakuna tena zimebaki wilaya chache, kwa mfano ugonjwa wa matende na mabusha tumebaki na wilaya 9, na tunaamini tukiendelea hivi ikifika mwaka 2030 tunaweza tukawa tumepunguza magonjwa kwa kiasi cha kutangaza kwamba Tanzania magonjwa haya siyo tena mzigo katika mfumo wa Afya"

Wilaya ambazo bado Magonjwa haya yapo ni pamoja na Ilala, Kinondon, Temeke, Mtama, Lindi, Mafia, Kilwa, Pangani na Mtwara Mikindani.

Pia Prof. Mgaya ameendelea kuwasisitiza wananchi wote kufuata maelekezo yote yanayotolewa na wataalamu wa Afya na inapofikia wakati wa kutoa kinga tiba zinazosambazwa wasiache kumeza kingatiba.

Kwa upande wake Mwakilishi wa taasisi ya utafiti wa kimataifa (RTI) kutoka Marekani, Dkt. Upendo Mwingira amesema wamekua wakifanya tathmini kwa kushirikiana na wizara ya afya na wadau kutoka NIMR ili kuweza kujua kingatiba wanazozitoa zina matokeo gani.