TANZANIA, KOREA KUSINI ZASHIRIKIANA KUIMARISHA HUDUMA ZA AFYA NGAZI YA MSINGI
Posted on: May 14th, 2024
Na WAF - Dodoma
Tanzania na Korea zimeendelea kufanya uboreshaji wa huduma za Afya ngazi ya Msingi, mifuko ya kikapu, ufadhili wa Moja kwa Moja wa Kituo cha Afya, huduma za afya ya uzazi kwa mtoto mchanga hali iliyo changia kupunguza viwango vya vifo vitokananvyo na uzazi kutoka 556 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000.
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema hayo leo Mei 14, 2024 wakati wa kikao na Wabunge kutoka Jamhuri ya Korea Kusini kilichofanyika ofisi za Wizara Jijini Dodoma baada ya kufanya ziara katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Upanga na Mloganzila ambapo wameridhishwa na huduma zinazotolewa na Hospitali hizo.
“Faida nyingine za ushirikano baina ya Tanzania na Korea Kusini ni uwekaji wa mtambo wa Oksijeni kwenye vituo vya afya ambao ulipunguza gharama ya kujaza mitungi ya oksijeni ambayo iliboresha ubora wa utoaji wa huduma kwa watoto wachanga na wajawazito,” amesema Mhe. Ummy
Aidha, Waziri @ummymwalimu ameiomba Korea iendelee kutoa msaada wa upanuzi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa, Amana, Temeke pamoja na Mwananyamala kufuatia ongezeko la wagonjwa na huduma zinazotolewa katika hospitali hizo ziendane na mahitaji ya sasa.
Kwa upande wake Mhe. Shin Hyun Young ambae ni Mbunge na Katibu wa Bunge la Korea amesema Walifurahishwa baada ya kufanya ziara zao, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Upanga na Mloganzila kwa kufanya kazi kwa ufanisi baada ya kuwakuta wagonjwa wengi na kufanya nao mahojiano ambapo walikiri kuwa huduma zinazotolewa kwa sasa ni nzuri.
Amesema, Korea Kusini ina uzoefu wa miaka 30 katika eneo la utekelezaji wa huduma za afya hususan Bima ya Afya kwa wote ambayo Tanzania inaweza ikajifunza mengi kupitia Mashirikaino yaliyopo kati ya Tanzania na Korea.
Waziri Ummy ametumia fursa hiyo kuwaomba Wabunge hao kukutana na wataalam wa Wizara ya Afya wa Tanzania pamoja na Wataalam wa masuala ya Afya wa Bima kutoka Korea ili wataalam hao waweze kujifunza zaidi kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote ilivyofanikiwa nchini Korea.