Wizara Ya Afya

TANZANIA, KOREA KUENDELEA KUSHIRIKIANA KUIMARISHA HUDUMA ZA MAABARA YA TAIFA

Posted on: October 22nd, 2026

Na Zakayo Mosha, WAF – Dar es Salaam

Wizara ya Afya kupitia Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii (National Public Health Laboratory – NPHL), kwa kushirikiana na Shirika la Korea Foundation for International Healthcare (KOFIH), inaendelea kutekeleza mradi wa miaka mitano unaolenga kuimarisha miundombinu ya maabara na kuwajengea uwezo watumishi katika usimamizi na udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza ili kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa Watanzania.

Akizungumza Oktoba 22, 2026, jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Huduma za Uchunguzi na Vifaa Tiba kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Alex Magesa, akimwakilisha Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Bruno Sunguya, katika kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mradi huo, amesema Maabara ya Taifa ni eneo muhimu katika ulinzi wa afya ya wananchi, hususan katika uchunguzi wa magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza.

Dkt. Magesa ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Korea kupitia KOFIH kwa kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya katika kuboresha miundombinu, vifaa na vitendea kazi vya Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii ili kuongeza uwezo wa nchi katika kugundua na kukabiliana na magonjwa mbalimbali.

Amesema kikao hicho ni muhimu katika kupata taarifa za hali halisi ya utekelezaji wa mradi, kutathmini maendeleo yaliyofikiwa, kubaini changamoto zilizopo na kuweka mikakati ya pamoja ya kuzitatua ili kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa ufanisi na kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Aidha, Dkt. Magesa amewahimiza wananchi kutoa taarifa kwa wakati kwa wataalamu wa afya wanapoona dalili zinazoweza kuashiria magonjwa mbalimbali, hususan katika kipindi ambacho dunia na bara la Afrika vinakabiliwa na hatari ya milipuko ya magonjwa, ikiwemo Ebola, ili kuwezesha hatua za haraka za uchunguzi na udhibiti kuchukuliwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii, Dkt. Peter Mbelele, amesema mradi huo ulianza mwaka 2023 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2028, ukiwa na lengo la kuimarisha miundombinu ya maabara pamoja na kuongeza ujuzi na uwezo wa watumishi katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.