Wizara Ya Afya

TANZANIA, DENMARK KUENDELEZA USHIRIKIANO KUIMARISHA SEKTA YA AFYA

Posted on: October 26th, 2026

Na Hassan Kimweri, WAF – Dar es Salaam

Ushirikiano wa muda mrefu kati ya Serikali ya Tanzania na Denmark umechangia maendeleo ya sekta ya afya nchini, hususan katika huduma za afya ya msingi, upatikanaji wa dawa na vifaa tiba pamoja na ufuatiliaji wa magonjwa.

Katibu Mkuu wa Wizara Afya Dkt. Grace Magembe, amesema hayo leo Oktoba 26, 2026 kwenye kikao, kati yake na Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Mhe. Jasper Kammersgaard, kilichofanyika katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya jijini Dar es Salaam ambapo amesema ushirikiano huo pia umeimarisha huduma za afya ya mama, mtoto mchanga na watoto.

"Kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, tunaishukuru Serikali ya Denmark kwa mchango wake katika kuimarisha Bohari ya Dawa (MSD), ambayo imepewa nafasi ya kuwa taasisi ya kikanda ya ununuzi wa bidhaa za afya kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)," amesema Dkt. Magembe

Aidha, Dkt. Magembe amesema Tanzania imepiga hatua katika ufuatiliaji wa magonjwa ya kuambukiza, huku akieleza kuwa usugu wa vimelea dhidi ya dawa (AMR) ni changamoto inayohitaji ushirikiano wa pamoja ili kupunguza gharama za matibabu.

Vilevile, Dkt. Magembe amesema Tanzania na Denmark zinaweza kuimarisha ushirikiano katika tafiti za kisayansi, ufuatiliaji wa magonjwa na udhibiti wa dawa na vifaa tiba, akibainisha kuwa taasisi za utafiti kama NIMR na MUHAS zina nafasi muhimu katika kuzalisha ushahidi wa kuboresha sera na huduma za afya.

Pia, Dkt. Magembe amesisitiza kuwa Serikali iko tayari kuendeleza na kurasimisha ushirikiano huo kwa kuzingatia vipaumbele vya taifa na umiliki wa ndani, huku akihimiza Denmark kuendelea kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali na asasi za kiraia ili kuboresha afya za wananchi.

Kwa upande wake, Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Mhe. Jasper Kammersgaard, amesema nchi hiyo inaendelea kuimarisha ushirikiano wa sekta ya afya Tanzania kupitia 'Danida Investment Fund', ambayo gawio la uwekezaji wake katika Benki ya CRDB huchangia Mfuko wa Pamoja wa Sekta ya Afya.