TANZANIA, ALMA KUENDELEA KUIMARISHA USHIRIKIANAO KUTOKOMEZA MALARIA BARANI AFRIKA
Posted on: June 22nd, 2024
Na WAF - Dar Es Salaam
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano na Taasisi ya Muungano wa Viongozi wa Bara la Afrika katika kudhibiti Malaria -ALMA ili kuhakikisha juhudi za pamoja zinafikiwa kutokomeza visa vipya vya ugonjwa huo.
Waziri Ummy amesema hayo leo 22.06.2024 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla fupi ya kumkaribisha Rais wa Guinea Bissau na Mwenyekiti wa ALMA Mhe. Umaro Sissoco alipotembelea Ofisi za taasisi hiyo, zilizopo jengo la CEEMI la NIMR, lilipo jijini Dar es Salaam.
Mhe. Ummy amesema juhudi za kupambana na Malaria Tanzania pia imekuwa ni nchi ya kwanza Barani Afrika kutoa mafunzo kwa Wabunge kuhusu matumzi ya Kadi ya alama za Viashiria vya Malaria (Malaria Score Cards) ambazo zinalenga kuhimiza utekelezaji, uwajibikaji, na upatikanaji wa rasilimali za kutokomeza Malaria.
Mhe. Ummy ameongeza kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika mapambano dhidi ya Malaria kutokana na mikakati madhubuti iliyojiwekea yenye kuleta matokea chanya katika kupunguza visa vipya vya Malaria kutoka asilimia 14.8 mwaka 2015, hadi kufikia asilimia 8.1 mwaka 2022.
“pamoja na mafanikio haya, bado tuna hatua ndefu za kuchukua katika kutatua changamoto ya fedha za kutekeleza mikakati ya kitaifa ya kutokomeza malaria, ndio maana kama nchi tumeanzisha Baraza la Kutokomeza Malaria Tanzania (EMC) litakalosaidia kuhamasisha upatikanaji wa fedha na bidhaa za afya na hivyo kupunguza uagizaji wa bidhaa hizo kutoka nje ya nchi.” Amefafanua Mhe. Ummy