Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

"SHIRIKA LA MADAKTARI AFRIKA” LAISAIDIA JKCI VIFAA TIBA VYA BILIONI MOJA

Posted on: July 12th, 2023

Na. WAF Dar Es Salaam

Shirika la "Madaktari Afrika" lililopo nchini Marekani limetoa msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi bilioni moja ambavyo vitatumika katika kambi maalumu ya siku tano ya matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo wa watu wasiokua na uwezo.

Kambi hiyo ilianza katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ililenga kuwahudumia wagonjwa wasio kuwa na uwezo ambao wamefanyiwa uchunguzi na kupatiwa matibabu katika taasisi hiyo.

Licha ya kutoa vifaa tiba hivyo madaktari hao pia walibadilishana uzoefu baina ya wataalam wa afya wa JKCI na wenzao kutoka Shirika la Madaktari Afrika.

Alizungumza na madaktari wanaotoa matibabu katika kambi hiyo alipowatembela  jijini Dar es Salaam Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Godwin Mollel aliwashukuru Madaktari Afrika kwa msaada walioutoa na kusema magonjwa ya mfumo wa umeme wa moyo ni sehemu ngumu kwenye masuala ya tiba ya moyo hivyo amewapongeza madaktari hao kwa kuwa mstari wa mbele kushirikiana na wataalam wa JKCI kuokoa maisha ya watanzania.

“Rais wetu alishawekeza mtambo wa kisasa wa kutibu umeme wa moyo, upande wa suala la tiba tumejitahidi kupata wataalam wenye uwezo wa kutoa huduma bora kuendana na teknolojia iliyopo, hatuna budi kushirikiana nanyi kwani muda mrefu mmekuwa mkitoa matibabu haya”,  alisema Dkt. Mollel.

Dkt. Mollel alisema mbali na kubadilishana uzoefu madaktari hao wamekuja wakijua yakuwa kuna watanzania wenye matatizo ya umeme wa moyo lakini hawana uwezo wa kumudu gharama za matibabu hivyo kuleta vifaa vya matibabu kuwatibu wasiokuwa na uwezo wa kugharamia matibabu.

“Kupitia kambi hii wataalam wetu wataenda kubadilishana uzoefu na kuendeleza teknolojia katika kutoa huduma za matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo na kuifanya Taasisi hii kutambulika katika nchi nyingi zilizotuzunguka hivyo badala ya kuwapeleka wagonjwa wao barani Ulaya sasa wanasaini mikataba na JKCI ili wagonjwa wao watibiwe hapa nchini kutokana na uwezo wetu kupanda hadi kufikia asilimia 97”, alisema Dkt. Mollel.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema madaktari kutoka Shirika la Madaktari Afrika wamekuja na vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi bilioni moja ili kuwasaidia wagonjwa wasiokuwa na uwezo wa kugharamia matibabu hayo.

“Madaktari Afrika ni marafiki zetu ambao wamekuwa wakishirikiana nasi kwa muda mrefu, wamefika hapa kwaajili ya kuwajengea uwezo madaktari wetu na kuwasaidia wagonjwa wenye matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo kutokufanya kazi vizuri”, alisema Dkt. Kisenge.

Dkt. Kisenge alisema katika kambi hiyo wagonjwa wenye matatizo makubwa ya mfumo wa umeme wa moyo watapatiwa matibabu na mabingwa hao wakiwa na lengo la kutoa huduma za matibabu pamoja na kubadilishana uzoefu na madaktari, wauguzi na wataalam wa kuendesha mtambo wa Cathlab.

Naye, Daktari bingwa wa mfumo wa umeme wa moyo kutoka Shirika la Madaktari Afrika David Singh alisema katika kambi hiyo wanashirikiana na madaktari wa JKCI kujifunza mbinu mpya za matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo ili kuendana na maendeleo ya teknolojia ya matibabu.

“Tumefika katika Taasisi hii kwasababu tuna taarifa za huduma bora zinazotolewa kwa wagonjwa wanaotibiwa hapa, hivyo tukaona ni sehemu sahihi ambayo tunaweza kushirikiana na kuboresha huduma zaidi”, alisema Dkt. David.

Dkt. David alisema Shirika la Madaktari Afrika litaendelea kushirikiana na wataalam wa Afya wa JKCI kwani kwa sasa Taasisi hiyo inafanya vizuri katika utoaji wa uchunguzi na matibabu ya moyo Afrika Mashariki na kati.