Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SHILINGI MILIONI 500 ZATENGWA MRADI WA AFUA ZA UTAMBUZI WA SARATANI YA RETINA KWA WATOTO

Posted on: May 17th, 2024Na WAF - Mbeya.

Serikali kupitia Wizara ya Afya imetenga shilingi Milioni 500 kwa ajili ya Mradi wa kutekeleza afua za kuwezasha utambuzi wa mapema wa watoto wenye matatizo ya macho ikiwemo Saratani ya Macho katika Mikoa ya Kanda za nyanda za juu Kusini.

Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya akimuwakilisha Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu, Dkt. Elizabeth Nyema tarehe 17 Mei, 2024 kwenye maadhimisho ya wiki ya kuongeza uelewa kuhusu Saratani ya Macho kwa watoto “Retinoblastoma” yaliyofanyika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya.

Dkt. Nyema amesema Wizara ya Afya ipo katika hatua za mwisho kukamilisha mradi huo utakaotekelezwa kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia ngazi ya jamii hadi Hospitali za Kanda ambapo fedha zitakwenda kuboresha tiba kwa watoto hawa ili kuboresha uoni na kupunguza vifo vinavyotokana na saratani hiyo.

Aidha, Dkt. Nyema ameongeza kuwa jumla ya wagonjwa wa saratani ya retina 227 walionwa katika vituo vya afya kutolea huduma za afya nchini kwa mwaka 2023 ukilinganisha na wagonjwa 214 walioonwa mwaka 2022 kwenye hospitali ya ngazi ya rufaa za Mkoa na Msingi na kutoa wito kwa wazazi kuwawahisha katika vituo vya kutolea huduma za Afya watoto wao pindi waonapo dalili za ugonjwa huo.

Kwa upande wake mratibu wa Mpango wa Taifa wa Huduma za Macho Wizara ya Afya Dkt. Bernadetha Shilio amesema watoto jumla ya 120,000 walionwa mwaka 2023 kwenye kliniki za macho katika hospitali za rufaa za mikoa na ngazi ya Msingi kati yao asilimia 42 ni watoto walio chini ya miaka mitano, aidha watoto takribani milioni 3.2 wenye umri wa chini ya miaka mitano walionwa katika kliniki za kawaida za ngazi za msingi.