SHILINGI BILIONI 30.9 KUBORESHA HUDUMA ZA MATIBABU YA SARATANI KANDA YA KATI
Posted on: September 3rd, 2025
Na WAF, Dodoma
Mradi wa ujenzi wa kituo cha umahiri cha matibabu ya magonjwa ya saratani katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Benjamin Mkapa utakaogharimu Shilingi Bilioni 30.9, utaongeza wigo wa matibabu ya uhakika ya Saratani kwa wananchi wa kanda ya kati na mikoa ya jirani.
Hayo yamebainishwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango leo Septemba 3, 2025 katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa kituo cha mafunzo, matibabu ya saratani pamoja na uzinduzi wa kituo cha upandikizaji figo kwenye Hospitali hiyo.
"Takwimu zinaonesha ongezeko kubwa la wagonjwa wa saratani za aina mbalimbali kama shingo ya mlango wa kizazi, matiti, tezi dume na nyinginezo ambazo zinasababisha vifo vingi pale zinapochelewa kugundulika na kupata matibabu sahihi, hivyo wito wangu kwa Wizara ya Afya kusimamia kwa karibu mradi huu ili kuhakikisha ujenzi na usimikaji wa vifaa tiba unakamilika kwa wakati na wataalam wa kutosha wanakuwepo," amesema Dkt. Mpango.
Pia Dkt. Mpango ametoa wito kwa Wizara ya Afya kutoa elimu kinga ya afya kuhusu chakula na lishe bora na mazoezi stahiki ya viungo kwa ubunifu na kuhakikisha elimu hiyo inahusisha shule, vyuo taasisi za kidini, mashirika yasiyo ya kiserikali na taasisi zingine za kijamii ili kuongeza jitihada za kutoa elimu hiyo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe, amesema Serikali ya awamu ya sita imefanya mageuzi makubwa ya kuimairsha huduma za afya nchini kuanzia ngazi ya msingi hadi taifa.
"Zaidi ya Shilingi Trilion 1.3 zimetumika katika maboresho ya miundombinu na vifaa tiba kwenye sekta ya afya ambayo imechangia mafanikio makubwa ikiwemo kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kutoka 556 hadi vifo 104 katika kila vizazi hai 100,000 kwa taarifa za mwaka 2022," amesema Dkt. Shekalaghe.
Kukamilika kwa mradi utaongeza upatikanaji wa matibabu ya uhakika ya saratani kwa wananchi wa kanda ya kati na jirani kwani kwa sasa matibabu ya uhakika ya ugonjwa huo yanapatikana katika hospitali ya Ocean Road jijini Dar es Salaam na Bugando jijini Mwanza.