Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SHERIA YA BIMA YA AFYA KWA WOTE KUANZA KUTUMIKA KABLA YA MWISHO WA APRIL, 2024

Posted on: April 3rd, 2024



Na. WAF, Dodoma

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema kuwa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote itatangazwa kuanza kutumika kabla ya Mwisho wa Mwezi wa Nne Mwaka 2024 kwa tarehe itakayotajwa.

Dkt. Mollel amebainisha hayo leo kwenye Bunge la 12, Mkutano wa 15 na kikao cha kikao cha pili wakati akijibu swali Namba 27 kutoka kwa Mbunge wa Viti Maakum Mhe. Furaha Ntengo Matondo aliyeuliza Je, lini Bima ya Afya kwa Watu Wote itaanza kutumika.

Dkt. Mollel amesema Serikali imeanza maandalizi ya kuanza kutumika kwa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ambapo kwa Mujibu wa Kifungu cha 1 cha Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote Waziri anaweza kuteua Baadhi ya Vifungu vya kuanza kutumika.

“Baadhi ya Vifungu ambavyo vinaweka Mifumo imara ya kutekeleza Bima ya Afya kwa Wote vimeshaainishwa na kuwasilishwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Sheria itatangazwa kuanza kutumika kabla ya Mwisho wa Mwezi wa Nne Mwaka 2024 kwa tarehe itakayotajwa”, ameeleza Dkt. Mollel.

Dkt. Mollel amesema kuwa serikali imeshaainisha vyanzo vitakavyo hudumia watu wasio kuwa wa uwezo wakiwemo wajane na watoto wa mitaani

Ikumbukwe Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ilipitishwa na Bunge tarehe 1 Novemba, 2023 na Mheshimiwa Rais ameidhinisha Sheria hiyo tarehe 19 Novemba, 2023 na imechapishwa katika gazeti la Serikali la tarehe 1 Desemba, 2023.