Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SHERIA YA BIMA YA AFYA KWA WOTE IKIDHI MATAKWA YA WATANZANIA

Posted on: January 21st, 2025

Na WAF - Dodoma

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati ikielekea kutekelea sheria ya Bima ya Afya kwa wote, Wajumbe wa Bodi mpya ya Wakurugenzi ya Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) wametakiwa kuhakikisha sheria hiyo inakidhi matakwa ya Watanzania wote.

Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hayo leo Januari 21, 2025 wakati akizindua Bodi mpya ya Wakurugenzi ya Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) ikiongozwa na Mwenyekiti wake Bw. Eliudi Sanga yenye wajumbe Nane akiwemo Katibu wa Bodi ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Dkt. Irene Isaka.

"Tunapozindua bodi hii naomba mbebe jukumu hili kubwa la kuhakikisha sheria ya bima ya afya kwa wote inatekelezeka kwa kuhakikisha kuwa inakidhi matakwa ya Watanzania wote ili wapate huduma za afya bora na zenye viwango vya hali ya juu," amesema Waziri Mhagama

Aidha, Waziri Mhagama ameitaka Bodi hiyo mpya kutafsiri kanuni na sheria za mfuko wa bima ya afya vizuri, pamoja na kujifunza kutoka kwa nchi zingine ambazo tayari zimefanikiwa kuendesha mfuko wa bima ya afya ili Tanzania iweze kufikia hatua nzuri ya uendeshaji wa mfuko wa bima ya afya.

"Watanzania wanategemea kupata usalama wa afya zao kupitia huduma bora za bima ya afya, hivyo ni matarajio yetu uzinduzi wa bodi yetu leo utaanza kazi haraka kuhakikisha huduma bora za afya kupitia bima ya afya zitapatikana kwa wepesi na haraka," amesema Waziri Mhagama

Katika hatua nyingine, Waziri Mhagama ameitaka bodi hiyo mpya kuhakikisha inatumia mapato yake vizuri kwa kazi zinazotambulika na thamani ya matumizi zinaendana na mapato, kufanya kazi kwa karibu na sekta binafsi.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Bw. Dany Temba, akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya ameitaka bodi hiyo kufanya kazi kwa haki na usawa kwakuwa imeaminiwa na kuchaguliwa kusimamia na kutafsiri kanuni na sheria za NHIF.