SERIKALI YAZINDUA MPANGO WA MACHO IMARA
Posted on: February 20th, 2025
Na WAF - Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI imezindua Mpango wa Macho Imara utakaohusisha upatikanaji wa huduma za awali za afya ya macho kwa watoto ili kukabiliana na changamoto ya ulemavu wa kutoona kwa watoto wachanga.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na ukunga Tanzania Bi. Ziada Sellah katika uzinduzi wa Mpango wa Macho Imara, wenye lengo la kuboresha huduma za macho kwa watoto chini ya miaka 15, uliofanyika jijini Dodoma Februari 20, 2025.
Bi. Sellah amesema takwimu zinaonesha kuwa watoto nane (8) kati ya 1000 wenye umri wa miaka sifuri (0) hadi 15 wanakabiliwa na ulemavu wa macho Tanzania, hali inayosababisha kukumbana na changamoto mbalimbali hasa katika makuzi na masomo yao.
"Magonjwa ya macho duniani yameongezeka kwa kasi, watoto wapatao milioni 1.4 wanakabiliwa na ulemavu wa kutokuona, zaidi ya asilimia 50 kati ya hao wanaishi katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania," amesema Bi. Sellah.
Ameongeza kuwa ili kukabiliana na changamoto hiyo, Mpango wa Macho Imara umezinduliwa rasmi ukilenga kuongeza upatikanaji wa huduma za awali za afya ya macho kwa watoto katika ngazi zote za huduma ya afya nchini.
“Magonjwa haya yanaweza kuzuilika na kutibika iwapo matibabu yataanza mapema, hivyo mradi huu utasaidia kuongeza wigo wa huduma za awali za afya ya mama na mtoto kwa kutambua matatizo ya macho mapema na kuyapatia tiba,” amesema Bi. Sellah.
Mpango huo utaanza kutekelezwa katika mikoa minne ya Manyara, Tabora, Arusha na Singida ambao utajikita katika kuboresha huduma za msingi za afya ya mama na mtoto ili kuhakikisha matatizo ya macho yanatambuliwa mapema.