Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI YAWEKA MIKAKATI ENDELEVU KUWAFIKIA WALENGWA WA CHANJO YA HPV

Posted on: April 29th, 2024Na WAF – Dodoma

Serikali imeweka mikakati endelevu kuwafikia mabinti wenye umri wa miaka tisa hadi kuni na Nne wa Tanzania bara na visiwani ambao bado hawajapatiwa chanjo ya Saratani ya mlango wa Kizazi (HPV).

Hayo yamesemwa na Meneja Mpango wa Taifa wa Chanjo Dkt. Florian Tinuga Aprili 29, 2024 Katika kikao cha tathmini ya utolewaji wa dozi Moja ya chanjo ya Saratani ya mlango wa Kizazi na waratibu wa chanjo kutoka Wizara ya Afya mkoani Dodoma.

“Wasichana wenye umri wa miaka tisa hadi kumi na Nne wapatao Milioni 5,028,357 kwa Bara na Visiwani, ikiwa bara ni Milioni 4,841,298 na Visiwani laki 187,059 watafikiwa na chanjo hiyo kwa mikoa 31 na Halmashauri 195 kabla ya kufika Disemba mwaka huu.” Amesema Dkt. Tinuga

Dkt. Tinuga amesema lengo ni kuwafikia mabinti Millioni tano wa Tanzania nzima ambapo mpaka sasa zoezi hilo limeonyesha mafanikio makubwa licha ya kutokea changamoto nyingi kama mvua lakini wananchi na wasimamizi wameonesha muitikio mkubwa.

Aidha, Dkt. Tinuga amesisistiza ushirikishwaji wa Taasisi mbalimbali kama za kidini katika kuhamasisha na kuelimisha Jamii juu ya usalama wa chanjo ya HPV.

“Kitu ambacho tumekiona kutoka kwenye tathmini yote ni kwamba tulikua na watoto wengi tuliowapata shuleni ambao ni asilimi 87 na asilimia 13 wako nje ya shule ambao wote wamepatiwa chanjo dozi moja ya HPV.” Amesema Dkt. Tinuga

“Chanjo hii ni salama na hutolewa bure kwa walengwa kwa hiari na chanjo hiyo hupunguza uwezekano wa kupata saratani ya mlango wa kizazi inapatikana katika vituo vya kutolea huduma za Afya.” Amesisitiza Dk Tinuga.

MWISHO