SERIKALI YATOA HUDUMA ZA AFYA YA AKILI KWENYE VITUO 701 NCHI NZIMA
Posted on: April 16th, 2025
Na WAF, Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Afya imepanua wigo wa huduma za ushauri nasaha na afya ya akili zinapatikana katika vituo 701 vya kutolea huduma za afya kote nchini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kukabiliana na changamoto ya afya ya akili kwa vijana na umma wa Watanzania kwa ujumla.
Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Lucy John Sabu, leo Aprili 16, 2025 Bungeni jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel amesema huduma hizo zinapatikana katika hospitali za rufaa za mikoa pamoja na Hospitali ya Afya ya Akili ya Mirembe.
“Huduma hizi zinahusisha ushauri nasaha na kampeni za uhamasishaji ili kuwasaidia vijana na makundi mengine ndani ya jamii kukabiliana na matatizo ya afya ya akili,” amesema Dkt. Mollel.
Ameongeza kuwa Serikali imewajengea uwezo wataalamu 2,840 wa afya wakiwemo madaktari na wauguzi ili waweze kutambua na kushughulikia changamoto za magonjwa yasiyoambukiza, yakiwemo matatizo ya afya ya akili, kwa lengo la kufikia watu wengi zaidi,
Aidha, Serikali imeanzisha huduma ya kituo cha simu za miito (Call Centre) kupitia namba 115, ambayo wananchi wanaweza kupata ushauri wa afya ya akili kwa njia ya simu, hatua inayochochea kupunguza unyanyapaa na kurahisisha upatikanaji wa huduma.
"Serikali imeanzisha vituo 1,561 vya huduma rafiki kwa vijana katika mikoa yote, kupitia Mkakati Jumuishi wa Vijana (NAIA), ambavyo vinatoa huduma za afya ya akili kwa njia rafiki, inayozingatia mazingira ya vijana" amesema Dkt Mollel.
Dkt. Mollel amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika huduma za afya ya akili ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata msaada unaohitajika kwa wakati.