Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI YATENGA ZAIDI YA BILIONI SABA KUKARABATI KITUO CHA AFYA MAKOLE

Posted on: January 20th, 2025

Na WAF - Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Afya imetenga zaidi ya Shilingi Bilioni Saba za kitanzania kwa mwaka wa fedha 2024/25 kwa lengo la kukarabati Kituo cha Afya Makole ili kiwe cha ghorofa hali itakayo ongeza tija hususan ni huduma bora za afya ya mama na mtoto.

Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hayo leo Januari 20, 2025 alipofanya ziara kwenye Kituo cha Afya Makole akiwa ameambatana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Dkt. Tedros Ghebreyesus aliyefika kujionea huduma zinazotolewa katika kituo hicho.

"Tumekuja hapa Kituo cha Afya Makole na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Dkt. Tedros Ghebreyesus kwa lengo la kuona juhudi za Serikali za kuhakikisha kwenye kuokoa vifo vya mama na mtoto lakini pia miradi ambayo Serikali inaendelea kuisimamia," amesema Waziri Mhagama

Aidha, Waziri Mhagama amesema huduma za msingi ambazo zitakuwa zikitolewa katika kituo hicho ni pamoja na huduma ya uzazi ili kuendelea kuokoa vifo vya mama na mtoto kwani hadi sasa Serikali imepunguza vifo hivyo kutoka 556 kwa vizazi hai 100,000 hadi 104 kwa vizazi hai 100,000 ndani ya miaka minne.

"Kwahiyo hata katika ukarabati na ujenzi wa kituo hiki, unalenga katika kutekeleza azma hiyohiyo ya Serikali ya kuhakikisha tunakua hatuna vifo vya akina mama na watoto wakati wa kujifungua," amesema Waziri Mhagama

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Jiji la Dodoma, Dkt. Pima Sebastian ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha hizo kwa lengo la kukarabati kituo hicho na kuipongeza kwa kuhakikisha inawekeza ili wananchi wapate huduma bora za afya.

"Tunashukuru kwa kutembelewa na ugeni huu mkubwa ukiongozwa na Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama aliyeambatana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani Dkt. Tedros Ghebreyesus kuja kuona huduma zinazotolewa katika kituo chetu cha afya Makole," amesema Dkt. Pima