Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI YAONGEZA MASHINE MPYA TATU ZA TIBA MIONZI

Posted on: July 29th, 2025

Na WAF - Dar es Salaam


Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan imenunua mashine mpya tatu za tiba mionzi kwa ajili ya kuboresha huduma za matibabu ya saratani nchini.


Dkt. Shekalaghe ametoa amesema hayo Julai 29, 2025 wakati wa ziara yake katika Taasisi ya Saratani Ocean Road, ambapo alieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali katika kutatua changamoto ya muda mrefu ya ucheleweshwaji wa huduma kwa wagonjwa kutokana na uhaba wa mashine hizo.


“Rais wenu mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ndiye aliyetoa fedha kwa ajili ya mashine hizi baada ya kusikia kilio cha wananchi kuhusu ucheleweshwaji wa huduma za mionzi kutokana na uhaba wa vifaa,” alisema Dkt. Shekalaghe.


Aidha, ametumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi kuwa wavumilivu wakati mashine hizo zikiendelea kufungwa na kuanza kutumika rasmi, huku akiwasihi kuendelea kushirikiana na watumishi wa afya.


Katika hatua nyingine, Dkt. Shekalaghe aliwapongeza watumishi wa sekta ya afya kwa kujituma na kutoa huduma kwa weledi mkubwa licha ya changamoto mbalimbali zinazowakabili.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road, Dkt. Diwani Msemo, alitoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwezesha upatikanaji wa mashine hizo za uchunguzi na matibabu katika taasisi hiyo, akisema kuwa hatua hiyo itaongeza kasi na ufanisi katika kuhudumia wagonjwa wa saratani.