Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI YAITAKA JAMII KUCHUKUA TAHADHALI DHIDI YA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA

Posted on: November 16th, 2024

Na WAF, Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Afya imetoa wito kwa jamii kuchukua hatua stahiki kuzuia ugonjwa wa kisukari na magonjwa mengine yasiyoambukiza kwa kubadili mtindo wa maisha.

Wito huo umetolewa Jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu, Wizara ya Afya Bw. Issa Ng’imba kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. John Jingu wakati wa kufunga kikao kazi cha wakurugenzi wa utawala, rasilimali watu, wakurugenzi wa sera, kujadili namna ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza mahali pa kazi.

Bw. Ng’imba amesema kuwa ipo haja ya kila mtanzania kuchukua hatua stahiki ili kuzuia ugonjwa wa kisukari kwa kubadilisha mtindo wa maisha na kuzingatia ulaji unaofaa, wenye kujumuisha mlo wenye mboga mboga, matunda nafaka zisizokobolewa na kuepuka ulaji wa vyakula vyenye sukari nyingi, chumvi nyingi na mafuta mengi.

Bw. Ng’imba amesema kutokana na ukubwa wa tatizo la magonjwa yasiyoambukiza nchini ipo haja ya kuongeza elimu kwa umma kuhusu njia za kuzuia magonjwa yasiyoambukiza na kuhimiza mabadiliko ya mtindo wa maisha kama kufanya mazoezi mara kwa mara, kuacha ulaji usiofaa na tabia bwete.

“Magonjwa yasiyoambukiza yanachangia kiwango kikubwa cha vifo na kupunguza ubora wa maisha ya watu na kuathiri familia, jamii na uchumi kwa ujumla, hivyo basi ni jukumu letu kuhakikisha tunaweka sera na mikakati thabiti ili kuzuia, kugundua mapema na kutibu magonjwa haya kwa wakati,” ameeleza Bw. Ng’imba

Aidha amesema magonjwa yasiyoaambukiza kama shinikizo la damu, saratani, magonjwa ya kinywa na meno, kisukari na changamoto za afya ya akili yanahitaji hatua za haraka na za pamoja ili kuhakikisha taifa linakuwa salama.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Wizara ya Afya Dk.Hamad Nyembea, amesema kikao hicho cha siku mbili kilikuwa na lengo la kuimarisha mikakati ya kudhibiti ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza ambayo yameendelea kuwa changamoto kubwa katika jamii duniani kote.

“Lengo la kushirikisha wizara 15 ni kutokana na magonjwa yasiyoambukiza kuwa mtambuka ambapo tunahitaji ushiriki wa wizara zote kukabiliana na changamoto hii.