SERIKALI YAFANYA MAGEUZI MAKUBWA AFYA YA KINYWA NA MENO
Posted on: September 25th, 2025
Na WAF - Dododma
Serikali imefanikiwa kutekeleza mageuzi makubwa katika mfumo wa huduma za Afya ya Kinywa na Meno kuanzia mwishoni mwa mwaka 2022 hadi sasa, lengo likiwa ni kuboresha afya ya kinywa kwa wananchi wa Tanzania ili kuendana na viwango vya kimataifa kwa kutumia afua na tafiti mbalimvali za kisera.
Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa hivi karibuni kwenye jarida la kimataifa la Afya ya Kinywa na Meno (International Journal of Dentistry), baadhi ya mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na ununuzi wa viti vya kisasa vya meno 340, usimikaji wa mashine za kiradiolojia za kidijitali za meno 306 pamoja na uanzishwaji wa kadi ya alama ya Afya ya Kinywa (Oral Health Score card) ambayo inafuatilia na tathmini vipimo na utendaji wa huduma za afya ya Kinywa na meno kwa vituo vya kutolea huduma kwa kipindi cha kutoka mwaka 2022-2024.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa uboreshaji huo umechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza uwiano wa kung’oa meno dhidi ya kutibu kutoka 2.8:1 mwaka 2022 hadi kufikia 1.3:1 mwaka 2025, kwa sasa dawa ya jino sio kung'oa ni kulitibu.
Pia, imeeleza kuwa Serikali imeanzisha huduma za Afya ya Kinywa na Meno kwa kina mama wajawazito ambapo mafunzo maalum hutolewa kwa wauguzi wafanyao kazi katika kliniki za wajawazito, kutoa elimu, kufanya uchunguzi na kutoa rufaa kwa kina mama wajawazito wote watakaogundulika na changamoto ya Magonjwa ya Kinywa na Meno. Mafanikio haya ya Serikali katika kuboresha huduma za kinywa na meno yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na mshikamano wa kisera, nia dhabiti ya kisiasa na ujumuishaji wa huduma hizi katika mfumo wa afya ya msingi.
Tanzania sasa inaonekana kama mfano wa kuigwa kwa nchi nyingine zinazoendelea katika kuimarisha huduma za afya ya kinywa na meno kwa usawa na njia endelevu.