Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI YAENDELEA KUCHUKUA TAHADHARI DHIDI YA MAGONJWA YA MLIPUKO

Posted on: October 12th, 2024

Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa ya mlipuko ikiwa ni pamoja na Mpox na Marburg.

Akizungumza na wataalamu wa Afya wa Uwanja Ndege na Bandari Oktoba 11, 2024 jijini Mwanza, Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. John Jingu amesema, kama nchi inachukua tahadhari na jitihada za makusudi ili kuepuka magonjwa haya.

"Nchi haina ugonjwa wa Mpox wala Marburg, moja ya jitihada tunazoendelea kuzifanya ni kuhakikisha tunaimarisha afya mipakani, tukimaanisha kila anayeingia nchini, kwa kujua hali yake ya kiafya, endapo ana changamoto yoyote inayofanana na hizi tunachukua hatua stahiki na za haraka," amefafanua Dkt. Jingu.

Ameeleza pia kuwa Serikali inawahimiza maafisa wa Afya kuendelea kutoa elimu na tahadhari juu ya magonjwa ya mlipuko hususani kwa hawa wanaosafiri nje ya mipaka kwa kutumia njia ya anga na ziwa.

Ametoa rai kwa wananchi wanaoishi mipakani kuwa, ni wajibu wa kila mtu kujua dalili za magonjwa haya na kutoa taarifa kwa wataalamu wa afya ili chukua hatua za haraka.

"Serikali imejenga uwezo wa wataalamu wa afya mipakani ambao wana vifaa na nyenzo za kubainisha changamoto kama hizo na pia tuna Maabara ya Afya ya Taifa yenye uwezo wa kupima na kubaini changamoto zozote zinazojitokeza," ameeleza Dkt. Jingu.