Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI YAAGIZA MAJENGO YA DHARURA NA WAGONJWA MAHUTUTI HOSPITALI YA MANYARA KUANZA KUTOA HUDUMA

Posted on: November 29th, 2025

Na WAF- Manyara

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, ameagiza kuanza kutumika kwa majengo mapya ya dharura na wagonjwa mahututi (ICU) katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Manyara, baada ya mradi huo kufikia zaidi ya asilimia 90 ya ujenzi.

Dkt. Samizi ametoa maagizo hayo Novemba 26, 2025 akiwa katika ziara yake mkoani Manyara yenye lengo la kukagua miradi ya afya pamoja na kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa wakati bila kusubiri kukamilika kwa kazi ndogo ndogo zinazoendelea.

"Jengo la dharura limefikia asilimia 94 ya ujenzi, jengo la wagonjwa mahututi asilimia 96, huku jengo la Benki ya Damu Salama likiwa asilimia 75, huku majengo mawili yakiwa yamezidi asilimia 90 yaanze kutumika mara moja ili kurahisisha huduma kwa wagonjwa" amesema Dkt.Samizi.

Ameongeza kuwa vyumba vya wagonjwa mahututi na dharura ni muhimu sana, hivyo, shughuli ndogo ndogo haziwezi kuzuia utoaji wa huduma muhimu, huku akielekeza ujenzi wa jengo la damu salama uendelee haraka na kukamilika kwa wakati.

Aidha, amewataka wasimamizi wa hospitali na wakandarasi kuongeza kasi ya ukamilishaji wa miradi hiyo ili kuhakikisha wananchi wa Manyara wanapata huduma bora na za uhakika.