Wizara Ya Afya

SERIKALI, WHO KUIMARISHA UTAYARI WA KUKABILIANA NA TISHIO LA UGONJWA WA EBOLA

Posted on: October 27th, 2026

Na Hassan Kimweri, WAF – Dar es Salaam

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe, leo Oktoba 27, 2026, amekutana na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini Tanzania, Dkt. Alex Ntale Gasasira, kujadili mikakati ya kuimarisha maandalizi ya kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola na kuimarisha mifumo ya afya nchini.

Mazungumzo hayo yaliyofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Afya jijini Dar es Salaam, yamelenga kupitia na kuimarisha hatua za maandalizi ya dharura, kwa kuzingatia hali ya mlipuko wa ugonjwa huo kwa nchi jirani.

Katika kikao hicho, viongozi hao wamejadili mapitio ya mpango wa dharura (Contingency Plan), kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa na mifumo ya utoaji wa tahadhari za mapema, pamoja na upatikanaji na utoaji wa chanjo.

Aidha, wamejadili tathmini ya utayari wa mikoa ili kukabiliana na mlipuko, ikiwemo upatikanaji wa vifaa vya kujikinga, uwezo wa timu za mwitikio wa haraka, ufuatiliaji wa watu waliokutana na wagonjwa na maandalizi ya vituo vya kutenga wagonjwa.

Vilevile, mazungumzo hayo yameangazia umuhimu wa kuimarisha uratibu wa rasilimali na uwajibikaji wa wadau kupitia Kikosi Kazi cha Taifa, ili kuhakikisha maandalizi na hatua za kukabiliana na mlipuko zinatekelezwa kwa ufanisi.

Kuhusu kuimarisha kinga dhidi ya maambukizi kutoka nje ya nchi, viongozi hao pia wamejadili kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na WHO, hususan katika kuboresha ufuatiliaji katika maeneo muhimu ya kuingia nchini, ikiwemo bandari.

Hatua hizo zinalenga kuimarisha utayari wa sekta ya afya, kuzuia kuingia na kuenea kwa maambukizi na kulinda afya za wananchi dhidi ya milipuko ya magonjwa ya kuambukiza.