SERIKALI, WADAU WAKUTANA KUJADILI UIMARISHAJI SEKTA YA AFYA NCHINI
Posted on: July 25th, 2025
Na WAF, Dodoma.
Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais TÀMISEMI, wamekutana na wadau kutoka Shirika la Kimataifa la masuala ya Afya la Korea (Korea Foundation for International Healthcare-KOFIH) kujadili mikakati ya pamoja itakayowezesha taasisi hiyo kuendelea kutoa ufadhili ili kuimarisha sekta ya afya nchini.
Akifungua warsha hiyo Julai 24, 2025 jijini Dodoma, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Afya Bw. Amour Amour amesema warsha hiyo inadhihirisha wazi ni jinsi gani taasisi ya KOFIH iko tayari kushirikiana na Serikali kwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya.
“Tumekutana hapa tukiwa na maono ya pamoja ya kuhakikisha kuwa mifumo ya sekta ya afya inaimarishwa ikiwa ni pamoja na rasilimali watu miundombinu na ubunifu,” amefafanua Bw. Amour.
Amesema kuwa Tanzania iko kwenye hatua za mabadiliko katika sekta ya afya hivyo kama nchi haiwezi kufanya mabadiliko haya bila kuwa na ushirikiano na wadau kama KOFIH ambao wamekuwa ni msaada mkubwa katika kuimarisha huduma za afya nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa KOFIH Bw. Gyeongbae Seo amesema taasisi yake inaahidi kuendelea kuimarisha sekta ya afya nchini ikiwa ni pamoja na kugharamia mafunzo kwa wataalam wa afya na kuboresha miundombinu ya sekta ya afya utakaowezesha utoaji wa huduma bora za afya.
Miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa katika warsha hiyo ni pamoja kuimarisha mifumo ya afya kupitia ushirikiano wa kimkakati, kuwekeza katika rasilimali watu, miundombinu na ubunifu.