SERIKALI, WADAU WAJADILI VIPAUMBELE VYA SEKTA YA AFYA - 2025/26
Posted on: April 9th, 2025
Na. WAF, Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ya Sekta ya Afya imeendelea kuweka vipaumbele katika Sekta ya Afya kwa mwaka wa fedha 2025/26 ili kuendelea kuimarisha utoaji wa huduma bora za Afya na kwa wakati kwa jamii.
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama ameyasema hayo Aprili 9, 2025 wakati akifungua mkutano wa 24 wa kisera wa Sekta Jijini Dodoma.
Waziri Mhagama amesema vipaumbele vya Sekta ya Afya kwa mwaka wa fedha 2025/26 ni kuhakikisha inakuwa na utoshelevu wa watumishi, ujenzi wa mifumo utakaosaidia ufuataliaji wa utoaji wa huduma bora na kuhakikisha Watanzania wote wanafikiwa na huduma kwa wakati na kwa kiwango cha juu.
“Vipaumbele hivi vitafuatwa na Serikali, wadau wa maendeleo na sekta binafsi na pia tutahakikisha bidhaa za afya zinazalishwa kwa wingi nchini Tanzania na kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji huo, vilevile kununua teknolojia ya vifaa tiba na vifaa vya uchunguzi ili tuweze kuzalisha nchini na tukifanya hivyo itaturahisishia sana suala zima la mnyoyoro wa utoaji wa huduma za afya kwa wananchi kwa kuzingatia kiwango tunachokitaka,” amesema Mhe. Mhagama.
Aidha, ameeleza eneo lingine ni kujiandaa na kuwa na njia za kudhibiti magonjwa ya mlipuko na magonjwa yasiyoambukiza kwa kuendelea kujikita kutoa elimu ya njia ya kujikinga na uwekezaji zaidi wa vifaa tiba na wataalam zaidi.
Ameongeza kipaumbele kingine ni usomeshaji wa wataalam wenye ubingwa na ubobezi kwenye maeneo ya kimkakati ambayo yanaujitaji mkubwa kwa wananchi kwenye baadhi ya magonjwa ambayo wananchi wanayafuata nje ya nchi ili matibabu hayo wayapate hapahapa Tanzania.
Awali akitoa salamu za Ofisi ya Rais-Tamisemi, Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi Dkt. Festo Dugange amesema Ofisi yake inaendeleea kushirikiana na wadau wa maendeleo ya sekta ya Afya na sekta binafsi katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi, magonjwa yasiyo ya kuambukiza ili kuendelea kuimarisha hali ya huduma za afya ngazi ya msingi.