Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI, WADAU KUSHIRIKIANA UANZISHAJI WA CHOMBO CHA KUSIMAMIA UBORA WA HUDUMA ZA AFYA

Posted on: September 25th, 2025

Na WAF – Dar es Salaam

Serikali Kupitia Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais -TAMISEMI imekutana na wadau kwa ajili ya kujadili na kuchukua maoni kuhusu rasimu ya uundaji wa sheria itakayowezesha kuanzishwa kwa chombo maalumu cha kusimamia ubora na kutoa ithibati kwa taasisi za afya nchini

Hayo yamebainishwa leo Septemba 23, 2025 na Mratibu wa Huduma za Utalii Tiba, Dkt. Asha Mahita, Jijini Dar es Salaam wakati wa uandaaji wa chombo cha kusimamia ubora wa huduma za afya.

Majadiliano hayo yamewakutanisha wataalam wa afya, wanasheria na watunga sera kutoka Wizara ya Afya pamoja na taasisi zinazohusika moja kwa moja na utoaji wa huduma za afya.

Dkt. Mahita amesema, kuanzishwa kwa chombo hicho ni hatua ya kimkakati itakayosaidia kuimarisha viwango vya ubora katika sekta ya afya na kupunguza gharama kubwa ambazo taasisi zimekuwa zikilipa ili kupata ithibati kutoka nje ya nchi.

“Hatua hii pia itaongeza imani ya wananchi kwa huduma zinazotolewa ndani ya nchi, kwani wananchi watakuwa na uhakika wa kupatiwa huduma bora zinazokidhi viwango vya kitaifa na kimataifa," amesema Dkt. Mahita.

Kwa upande wao, Mratibu wa ubora wa huduma kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Dkt. Pius Kagoma amepongeza mpango huo wakieleza kuwa chombo hicho kitakuwa nyenzo muhimu ya kuhakikisha taasisi zote za afya nchini zinatoa huduma bora zinazokidhi viwango vya kitaifa na kimataifa, huku kikiimarisha usimamizi endelevu wa sekta ya afya.

Dkt. Kagoma ametoa rai kwa wadau wote kuendelea kushirikiana katika hatua zinazofuata za uundaji wa sheria na kanuni zitakazosimamia chombo hicho, ili kuhakikisha kinakuwa imara, chenye ufanisi na manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi.