Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI .WADAU KUIMARISHA AFUA ZA KUPUNGUZA MAAMBUKIZI NA VIFO VYA KIFUA KIKUU

Posted on: November 17th, 2024

Na WAF - Dodoma

Wadau wa afya wamekutana kwa ajili ya kufanya mapitio ya hali ya ugonjwa wa kifua kikuu nchini, lengo likiwa ni kuboresha mikakati ya kupambana na kupunguza maambukizi yatokanayo na Kifua kikuu.

Hayo yamebainishwa leo Novemba 15, 2024 Mkoani Dodoma na Mkurugenzi Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Rashid Mfaume, wakati akifunga kikao cha wadau wa mapambano ya kifua kikuu kilichokutana kujadili kampeni ya kutafuta wagonjwa wa kifua kikuu.

Dkt. Mfaume amesema kuwa pamoja na mafanikio makubwa ambayo Serikali kwa kushirikiana na wadau imepata, bado kuna maeneo yanayokabiliwa na changamoto na yanahitaji mikakati jumuishi ili kutatuliwa. Amesema kuwa maeneo hayo ni pamoja na kutoa elimu na kuhamasisha uelewa wa magonjwa haya kwa jamii.

“Wagonjwa wa Kifua Kikuu sasa watapatiwa matibabu sambamba na kupatiwa huduma za ufuatiliaji na tathimini ya ufuasi wa dawa ili kuhakikisha wanamalizia matibabu yao kwa wakati wakiwa katika nchi hizo.” amesema Dkt. Mfaume.

Hata hivyo, Tanzania imepiga hatua katika kutokomeza ugonjwa wa kifua kikuu nchini kwa kuweza kupunguza maambukizi mapya ya kifua kikuu kwa asilimia 40 na vifo vitokanavyo na kifua kikuu kwa asilimia 67 kufikia mwaka 2023.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mikoa, Dkt. Bestie Magoma, amesema Serikali inaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha upatikanaji wa vifaa na dawa kwa gharama nafuu. Ufadhili wa rasilimali kutoka kwa wadau ni muhimu ili kupunguza ugonjwa wa kifua kikuu na kuboresha afya ya jamii.

“Ili kuboresha huduma kwa wagonjwa wa kifua kikuu, ni muhimu kuimarisha mifumo ya kidijitali kwa ufuatiliaji na kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya kuhusu usimamizi bora wa wagonjwa. Pia, kampeni za uhamasishaji zinahitajika ili kuwahimiza wagonjwa kufuata matibabu bila kukata tamaa,” amesema Dkt. Magoma.