SERIKALI KUZIDI KUIMARISHA UPATIKANAJI WA KONDOMU PEMBEZONI MWA NCHI.
Posted on: November 19th, 2024Na WAF - Dodoma.
Serikali imeazimia kuimarisha mnyororo wa ugavi na upatikanaji wa kondom nchini sambamba na utoaji wa elimu ili kuwafikia wananchi wote wenye mahitaji hadi maeneo ya pembezoni mwa nchi.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkuu wa Programu anayesimamia Ukimwi, Homa ya Ini na magonjwa ya Ngono Dkt. Kisonga Riziki Novemba 19, 2024, Jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa mkutano wa mwaka wa wadau wa afua jumuishi za kondomu.
Dkt. Kisonga amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha elimu juu ya matumizi inapatikana na kufikiwa na watu wote, kuendelea kupenya zaidi katika maeneo ya miji midogo na wilaya.
“Tumeadhimia Kuimarisha juhudi zetu za kukuza matumizi sahihi na endelevu ya kondomu kwa kutoa elimu zaidi kupitia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na elimu ya ana kwa ana, ni muhimu kuelimisha jamii kuwa kondomu ni kinga dhidi ya VVU, magonjwa ya ngono, mimba zisizotarajiwa na pia ugonjwa wa homa ya ini,” amesema Dkt. Kisonga.
Amesema Wizara imeendelea kuratibu manunuzi na usambazaji wa kondomu kupitia programu jumuishi ya kondomu ili kila kundi katika jamii liweze kutumia kondomu kulingana na uwezo au chaguo.
“Tunazidi kuhakikisha kwamba kondomu zinapatikana na kufikiwa na watu wote, hasa katika maeneo ya pembezoni na ambayo hayana huduma ya kutosha, kuendelea kupenya zaidi katika maeneo ya miji midogo na wilaya ili kutanua soko. kwa kipindi cha Januari 2023 hadi Oktoba 2024 Wizara imeagiza na kusambaza kondomu aina ya zana inayotolewa bila malipo kwa walengwa zipatazo171,665,200 zenye thamani ya Tsh. 14,014,217,787.19,” amesema Dkt. Kisonga.
Kwa upande wake Dkt. Zeye Masunga amesema kufuatia idadi ndogo ya matumizi ya kondomu wizara ya afya imeona umuhimu wa kuwa na kikao hicho ili kuangalia jinsi ya kufikia jamii kwa urahisi.