Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI KUZALISHA WAHUDUMU WA AFYA NGAZI YA JAMII 13,500 KILA MWAKA

Posted on: July 27th, 2022

Na. Majid Abdulkarim, WAF - MWANZA
Serikali kupitia Wizara ya Afya imesema kulingana na jumla ya idadi ya Vitongoji na Mitaa nchini, inatarajia kuwa na Wahudumu wa afya ngazi ya jamii 68,647 ili kufikia lengo ndani ya miaka mitano na kuzalisha wahudumu wa afya ngazi ya jamii (CHWs) wasiopungua 13,500 kila mwaka.

Kauli hiyo imebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel leo wakati wa Kikao kazi cha Wadau na Watekelezaji wa Afua za Afya Ngazi ya Jamii katika mkoa wa Mwanza ambapo amesema kwa takwimu zilizopo sasa, kufikia mwezi Juni, 2022 takribani Wahudumu Afya ngazi ya Jamii (CHWs) 10,524 wamepatiwa mafunzo kwa vipindi tofauti kati ya hao, wahudumu wa afya ngazi ya jamii 3,524 wamepata mafunzo ya Moduli ya kwanza na wahudumu wa faya ngazi ya jamii 7,000 walipata mafunzo mafupi ya UVIKO-19, Idadi hii haikujumuisha Wahudumu wanaokamilisha mafunzo yao leo.\

Akizungumza Mhandisi Gabriel ameipongeza Wizara ya Afya kwa kuendeleza jitihada mbalimbali zenye lengo la kuimarisha utoaji huduma ya Afya kwa wananchi akibainisha kwamba wahudumu hao 600 waliohitimu mafunzo ya wahudumu wa afya ngazi ya jamii ni nguzo muhimu katika kutoa huduma kwenye jamii.

Aidha amebainisha kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya imepanga kuandaa miongozo inayotumika hivi sasa katika sekta ya Afya ikiwa ni pamoja na Mwongozo wa Kisera wa Huduma za Afya ya Jamii mwaka 2020 na Mwongozo wa Kitaifa wa Utekelezaji wa Huduma za Afya ya Jamii (National Operational Guideline for Community-Based Health Services) uliosainiwa Desemba 2021.

Mhandisi Gabriel amewaeleza wadau wa Afya kwamba mnamo tarehe 7-8 mwezi Juni 2022 Mhe. Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya alishiriki kikao cha kimataifa kinachoitwa Global Financing Facility Investors Group Meeting kilichofanyika jijini Paris, Ufaransa.

Pia katika kikao hicho amewakumbusha wadau na wataalamu wa afya nchini uimarishwaji wa huduma za afya ya jamii ambapo suala hilo lilijadiliwa sambamba na umuhimu wa kuwa na Wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii.